Mchuano mkali kiti cha ubunge Kibamba

DAR ES SALAAM: MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mshauri wa Rais, Angela Kairuki, amewaomba wajumbe wa CCM kumpa ridhaa ya kugombea ubunge wa Jimbo la Kibamba katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa chama hicho katika mkutano maalum, Angela Kairuki ameeleza dhamira yake ya kuleta mabadiliko chanya katika Jimbo la Kibamba kwa kushirikiana na wananchi katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
“Nina dhamira ya dhati ya kushirikiana na jamii ya Kibamba kuboresha miundombinu, huduma za usafiri wa umma, sekta ya elimu kwa kupunguza msongamano wa wanafunzi, pamoja na kuinua vipaji vya michezo kwa vijana wetu,” amesema Angela.
Pia ameeleza mpango wake wa kusaidia wakina mama na vijana kwa kuwawezesha kuwapatia fursa za mitaji, pamoja na kukamilisha ujenzi wa zahanati zilizokwama ili kuboresha huduma za afya hasa kwa mama na mtoto.
Angela ameongeza kuwa atahakikisha wazee, wakiwemo wanaume, wanashirikishwa katika mikopo kwa kusisitiza serikali kuwazingatia katika mipango ya kiuchumi, huku akisisitiza ataendelea kuhakikisha wanawake wanapata mikopo kwa ajili ya maendeleo yao.
Kuhusu changamoto ya shule kuwa mbali na makazi ya wananchi, Angela ameahidi kuwa ataendelea kuisemea kwa serikali na kuhakikisha shule mpya zinajengwa karibu na wananchi ili watoto wasitembee umbali mrefu kupata elimu.
Katika sera zake nyingine, Angela Kairuki ameeleza lengo la kuwaunganisha vijana wa Kibamba kupata ajira serikalini, sekta binafsi na kuwawezesha kujiajiri kwa kutoa mafunzo na kuhamasisha ujasiriamali.
“Niko tayari kuunganisha nguvu na wananchi wa Kibamba kutekeleza yale yote yaliyoachwa njiani ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa wote,” ameongeza.
“Kama mtanipa ridhaa, nitafanya kazi bila kuchoka. Naombeni mnitime niwatumikie wananchi wa Kibamba,” amemaliza kwa kuisisitiza hivyo.
Kwa upande wake mbunge anaemaliza muda wake katika jimbo hilo Issa Mtemvu amesema katika ahadi alizotoa mwaka 2020 kwa asilimia kubwa amezitekeleza na chache zilizosalia anakwenda kuzimalizia ikiwa atapewa ridhaa kwa mara nyingine.
Akizungumza na wajumbe Mtemvu amesema ndani ya miaka minne na nusu aliyolitumikia jimbo hilo amefanya mambo mengi makuba yaliyokwama kwa muda mrefu.
“Ninyi mtakuwa mashahidi wakati ninaingia hali ya miundombinu ilikuwa hairidhishi lakini kwasasa tumeboresha maeneo mengi yana barabara za lami lakini si hivyo tu tumegusa pia sekta ya elimu tumejenga shule 12, shule tano za msingi na saba za sekondari” amesema Mtemvu na kuongeza kuwa
“Wakati naingia madarakani nilikuta miradi mingi ya maji inapita hapa bila kuwanufaisha wananchi wa hapa mfano mradi wa maji Kisarawe, nilipambana na kuhakikisha kuwa mnapata maji na leo wote mnashuhudia huduma nzuri ya maji niwaambie tu mengine ambayo hajakamilika nikipata ridhaa yenu kwa mara nyingine ninakwenda kukamilisha na kuja na mambo mengine mapya”.
Katika hatua nyingine Joseph Masatu ambaye nae ni mtia nia ya Ubunge katika Jimbo hilo amesema kipaumbele chake kikubwa ni miundombinu ambapo atahakikisha barabara zinazoelekea katika mitaa mbalimbali zinakuwa za kiwango cha lami huku akiahidi kuwa mstari wa mbele katika kuzisimamia kazi hizo.
Watia nia wengine ni Dk Alphonce Temba, Mwamini Mwambo, CPA. Consolatha Rweikiza, Dk Nestory Yamungu na Angelo Nyonyi.
Baada ya kukamilika kwa kampeni hizo, Agosti 4 mwaka huu wajumbe watapiga kura na kisha baadae majina yatarudishwa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo watataoa jina la mgombea mmoja atakaewakilisha chama hicho katika uchaguzi mkuu.