45 wafanyiwa upasuaji kambi ya Imamu Hussein

DAR ES SALAAM; WANANCHI 45 waliokutwa na tatizo la mtoto wa jicho kwenye kambi ya matibabu ya Imamu Hussein (AS) wamefanyiwa upasuaji bure.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Khoja Shia Ithninasher Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Mohammedraza Dewji, amesema  wananchi hao waliokutwa na tatizo la mtoto wa jicho wamefanyiwa upasuaji katika Hospital ya Medwell iliyopo kibaha mkoani Pwani inayomilikiwa na Jumuiya ya Khoja Shia Ithninasher Mkoa wa Dar es Salaam, iliyoandaa kambi hiyo.

Amesema kuwa mbali na kupimwa macho na kutolewa kwa miwani na dawa, pia kulikuwa na huduma za bure za upimaji wa afya na maradhi yasioambukiza ikiwemo shinikizo la damu na kisukari.

“Wananchi wengi walijitokeza kwenye kambi yetu, kwa leo inawezekana tusitoe takwimu sahihi kwa waliofanyiwa vipimo, ila kwa siku mbili za mwanzo waliofanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho na kupatiwa matibabu mengine bure ni 45,” amesema wakati akifunga kambi hiyo iliyofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Pia amesema kulikuwa na uchangiaji damu salama kwa kushiriiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama na upimaji wa kansa ya shingo ya kizazi na matiti kwa kina mama na tezi dume kwa wanaume, mambo yote yakiratibiwa na jumuiya hiyo.

Amesema  kambi hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na watu wengi  kupata huduma, ambapo ndivyo alikuwa akiishi  Imam Hussein (AS).

Alisema wastani kwa siku walikuwa wakihudumia wananchi 2000 kwa siku mbili za mwanzo, lakini siku ya mwisho walijitokeza zaidi ya wananchi 5,000.

Alitoa rai kwa wananchi wawe wanajitokeza siku za mwanzo ili kupunguzq idadi ya watu kuwa kubwa siku za mwisho wa kambi watakaposikia kuna huduma za upimaji wa afya na macho bure, basi ni vyema wakafika siku za mwanzo Ili kupata huduma.

Alisema kuwa mbali na kukutwa na changamoto ya mtoto wa jicho pia kuna watu wengine walipima na kukutwa na uono hafifu na kupewa miwani na wengine walipewa dawa za kutibu macho.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button