TFS yapewa kongole usimamizi hifadhi ya misitu

MOROGORO: WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umepongezwa kwa kazi nzuri ya uhifadhi wa misitu na jitihada kubwa wanazozifanya kufikisha elimu kwa wananchi ili wawe walinzi katika kudhibiti vitendo vya uchomaji moto misitu ya asili na ya hifadhi kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk Batilda Buriani amesema hayo alipotembelea banda la TFS kwenye maonesho ya Nannane Kanda ya Mashariki kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikishirikisha mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani na mwenyeji Morogoro.

Balozi Dk Buriani amesema  Wakala huo umekuwa ukifanya kazi  kubwa katika suala nzima la kuifanya Tanzania ya kijani inawezekana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye naye ‘mama champion’ wa mazingira namba moja.

“ Hawa zetu wa TFS wanafanya kazi kubwa na tumeona sasa hivi hata wimbi la uchomaji wa misitu umepungua kwa kiasi kikubwa , tuwapongeze kwa kazi hii wanayoifanya ya kulinda misitu, kuhifadhi mazingira na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya rasilimali misitu,” amesema Balozi Dk Buriani.

Balozi Dk Buriani amesema ni muhimu wananchi hasa wakulima na wafugaji kutembelea banda la Wakala huo ili kujionea teknolojia mbalimbali wanazotumia, kupata elimu kuhusu namna bora ya kuhifadhi mazingira, na hasa namna ya kujikinga dhidi ya moto mwitu ambao umekuwa tishio kwa misitu yetu.

Amesema wakala huo umekuwa ikifanya kazi ya kushirikisha vijana na makundi ya wakina mama ya kuwapa elimu ya kuongeza thamani katika mazao ya misitu na biashara nzima ya hewa ya ukaa ambayo sasa hivi imeshika hatamu.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu Ugani na Uenezi TFS Kanda ya Mashariki ,Shabani Kiulah, amesema kuwa wakala huo umekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi salama ya moto hasa wakati wa kuandaa mashamba ili kuepusha athari za moto mwitu kwa mazingira na misitu ya asili.

Kiulah amesema  katika  maonesho hayo  wanawapa wananchi mbinu na teknolojia za kisasa za uhifadhi na usimamizi wa misitu, njia sahihi za kuzima moto na jinsi ya kutumia moto kwa usalama bila kuharibu mazingira.

“ Tunawahimiza wananchi watembelee banda letu ili wajifunze zaidi na washiriki katika juhudi za kitaifa za kuhifadhi rasilimali za misitu,” amesema Kiulah.

Kiulah amesisitiza kuwa elimu inayotolewa na TFS si tu kwa wakulima na wafugaji, bali pia kwa wanafunzi na vijana wanaotembelea banda hilo, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha kizazi kijacho kujali na kulinda mazingira.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button