Waandishi Bunifu waalikwa kushiriki Tuzo ya Mwalimu Nyerere

DAR ES SALAAM : DURU ya nne ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2025/2026 imezinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam, huku waandishi wa habari wakihimizwa kujiandaa na kuwasilisha miswada yao kwa ajili ya kushiriki katika mchakato wa ushindani.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa huu ni wakati muafaka kwa waandishi wa habari kuwasilisha kazi zao za ubunifu  kwa Kamati ya Kitaifa ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, kwa lengo la kuendeleza jitihada za kukuza uandishi na matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini.

“Tuzo hii ni sehemu ya dhamira ya serikali kuendeleza urithi wa fikra na maono ya Mwalimu Nyerere kupitia lugha ya Kiswahili na uandishi wa ubunifu. Tunawakaribisha waandishi wote kushiriki kwa wingi,” alisema Prof. Mkenda.

Aliongeza kuwa kabla ya uzinduzi huo, serikali ilikutana na wadau wa sekta ya uandishi bunifu kujadili njia za kuboresha tuzo hiyo, ili kuhakikisha inaendelea kuwa bora na kuchochea usomaji wa vitabu pamoja na ukuzaji wa fasihi ya Kiswahili. SOMA: Jifunze Kiswahili

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Prof. Penina Mlama, alisema kuwa kwa mwaka huu, tuzo hiyo itaendelea kujumuisha kazi za Riwaya, Ushairi, Hadithi za Watoto na Ushairi wa Watoto, kama ilivyokuwa katika awamu ya mwaka 2024/2025.

“Mapokezi rasmi ya miswada yataanza tarehe 15 Agosti 2025 na kufungwa tarehe 30 Novemba 2025. Tunatoa wito kwa waandishi wa kazi bunifu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kuwasilisha miswada yao mapema,” alisema Prof. Mlama

.Tuzo hiyo imelenga kuibua na kuthamini vipaji vya uandishi, kukuza matumizi ya Kiswahili sanifu, na kuchochea hamasa ya usomaji miongoni mwa Watanzania wa rika zote.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button