Wajasiriamali Tandahimba wapongeza uwepo wa Nanenane

MTWARA: BAADHI ya wajasiliamali wadogo wanawake katika Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara wameipongeza serikali kwa kuendeleza maadhimisho ya nanenane kila mwaka nchini kwani yanawezesha wajasiliamali hao kukuza uchumi wao na kupanua wigo wa kazi zao.

Hayo yamejiri wakati wa maadhimisho ya maonyesho ya nanenane kanda ya kusini mwaka 2025 yaliyofanyika kwenye viwanja vya ngongo mkoani Lindi ambayo kila mwaka huanzia Agosti 1 hadi Agosti 8 na kushirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali zinazohusika na kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili.

Mjasiliamali anayejishughulisha na shughuli ya ubanguaji wa korosho ambaye ni mjumbe wa kikundi cha tulinge kilichopo kijiji cha mambamba wilayani humo, Tabizuna Mohamed amesema maonyesho hayo ni fursa kubwa kwao kwasababu yanawasaidia kupata wateja wengi kwa wakati mmoja hivyo kukuza uchumi kwa haraka.

‘’Tunapokuwa hapa tunauza sana bidhaa zetu mfano kikundi chetu kwa siku tunauza hadi korosho za takribani Sh 200,000  kule nyumbani kwa siku hata kufikia mauzo ya Sh 50,000 ni shida kwahiyo fursa hii ni muhimu sana kwetu pia inatusaidia  kupata masoko na kujulikana kuwa wapi tunapatikana na bidhaa zetu hizi’’amesema Tabizuna.

Pia ameishikuru halmashauri hiyo kwa kuwapatia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya  wanawake, vijana na walemavu kupitia mapato yake ya ndani ambapo inawezesha kukuza biashara zao kwani kikundi chao huko nyuma wameshawahi kupokea Sh milioni 5, Sh milioni 7, Sh milioni 10 na hivi karibuni wamepatiwa Sh milioni 8 huku kikundi kikiwa na wanachama 11.

Mjasiliamali mwingine ni Rukia Amri katibu mtendaji wa kikundi cha kulenga kilichopo kijiji cha milidu wilayani humo ambaye ni muuzaji wa bidhaa mchanganyiko ikiwemo matunda, mahindi, mtama, karanga, njugu mawe na zingine na mkulima wa mazao hayo, amesema jitihada hizo zote ni kupitia mikopo inayotolewa na halmashauri inawawezesha kuendeleza kilimo hicho.

‘’Tunawashukuru viongozi wetu kwa kutusimamia kututoa kule nyumbani kutuleta kwenye nanenane kwa ajili ya kutafuta soko pia kujifunza na baada ya kufika huku ni faida kubwa kwetu tunashukuru tumepiga hatua kwani tumetambulika na watu wengi na tunapata oda ya bidhaa zetu kutoka maeneo mbalimbali’’

‘’Kwa siku tangu tumefika tunafanya mauzo ya Sh 250,000 hadi Sh 300,000 na tumewahi kupata mkopo kupitia halmashauri mwanzo Sh 500,000 na hivi karibuni tumepata Sh milioni 8 na kwenye kikundi tuko wanachama 12 na mbali ya fursa za kiuchumi tunabadilishana mawzo na wenzetu wengine kama sehemu ya kujifunza na kuzidi kuongeza ujunzi wa kazi zetu ’’

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button