Waziri Kabudi azindua Bodi ya Wakurugenzi TSN

DAR ES SALAAM –– Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Palamagamba Kabudi, amezindua Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) yenye wajumbe saba akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni, Bi Asha Dachi.
Bodi hiyo itakayoongozwa na Mwenyekiti, Inspekta Jenerali wa Polisi mstaafu, Said Mwema, imeanza kazi rasmi baada ya kuzinduliwa leo Agosti 8, katika ofisi za Kampuni ya Magazeti TSN zilizopo Tazara, Temeke mkoani Dar es Salaam.
Hafla hiyo pia imehudhuliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
Wajumbe wa bodi hiyo ni pamoja na Dk. Chisugilie Salum Khadudu, Mkufunzi katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT); Joseline Jonathan Kamuhanda, Mkuu wa Kitengo cha Masoko, Benki ya CRDB; Dk. Ayub Rioba Chacha, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC); na Elimbora Abia Muro, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani katika Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA).
Wengine ni Deogratius Charles Kwiyukwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB); na Zamaradi Rashid Kawawa, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.