Wakulima washauriwa usindikaji wa muhogo

LINDI: WAJASILIAMALI katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara wameshauriwa kuhamasika na shughuli ya usindikaji wa muhogo ili kukuza uchumi zaidi.
Akizungumza na HabariLeo katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini yaliyofanyika katika viwanja vya ngongo mkoani Lindi, mmoja wa wajasiliamali kutoka wilayani humo Siajabu Lupanda kutoka kijiji cha mahuta amesema licha ya zao hilo la muhogo kuwapatia chakula lakini lina faida kubwa kwa biashara.
Aidha mjasiliamali huyo ambaye pia ni mkulima na msindikaji wa muhogo amesema muhogo una faida mbalimbali ikiwemo suala la chakula pamoja na biashara ambapo ni mbadala ya mazao mengine ya biashara yanayolimwa wilayani humo kama vile korosho, ufuta na mengine.

Kuhusu ushiriki wake katika maonesho hayo, amesema hatua ya yeye kuwa miongoni wajasiliamali yaliyoshiriki nanenane kutoka wilayani humo ni hatua kubwa kwake kwakuwa anapata kufahamika na watu kutoka maeneo tofauti tofauti ndani na nje ya kanda hiyo hivyo anakuza biashara yake inayomwezesha kuendesha majukumu ya kifamilia ikiwemo kusomesha watoto.
‘’Mimi ni msindikaji na mjasiliamali wa unga wa muhogo, muhogo ni zao lenye tija kwasababu ni chakula na biashara kwa ujumla kwahiyo kazi hii ndiyo iliyoniwezesha mimi kufika hapa nanenane na hizi ni jitihada za halmashauri kutuwezesha kupata mikopo hadi leo tuko hapa’’
Ameongeza kuwa, ‘’Pia niendelee kuwashauri wajasiliamali wenzangu tusitegemee kazi moja tu ujasiliamali kama vile ubanguaji wa korosho tu bali tujikite pia kwenye usindikaji wa muhogo kwasababu ni biashara ambayo pia ina faida kiuchumi’’amesisitiza Siajabu
Amezungumzia faida aliyoipata katika maonesho hayo ikiwemo mauzo ya uhakika ambayo kwa siku anauza unga wa muhogo takribani kilo 20 huku kilo moja ikiwa ni Sh 2,500, kuuza miche ya mihogo ambayo imekuwa na oda kubwa kwa watu kutoka maeneo mbalimbali wanaokuja kwenye banda hilo lao la maonesho la halmashauri ya wilaya ya Tandahimba.
‘’Kupitia faida tunazozipata sisi wajasiliamali kwenye maonesho haya, naishauri serikali kuwa maonesho haya yawe endelevu kwasababu hizi siku tulizokuwepo kwenye maonesho sisi wajasiliamali tunaotoka kule vijijini tuendelee kupata masoko zaidi kupitia kazi yetu hii’’amesema Lupanda



