Vitendo 1,338 ukatili kijinsia vyaripotiwa Mtwara

MTWARA: JUMLA ya vitendo 1,338 vya ukatili wa kijinsia vimeripotiwa kwa nyakati fotauti mkoani mtwara kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2025.
Hayo yamejiri wakati wa kongamano la siku moja la mmomonyoko wa maadili na programu ya Jumuishi ya Taifa ya Malezi Mkuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM), lililofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani leo Agosti 13.
Kongamano hilo limekutanisha wadau mbalimbali mkoani humo wakiwemo vijana, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na wengine, lililoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na Kitovu cha Maendeleo Safi (KIMAS) pamoja na Mtandao wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Tanzania (TECDEN).
Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Theresia Ngonyani amesema vitendo hivyo ni vile vilivyoripotiwa na kuna vile ambavyo havijaripotiwa bado viko vingi huko nje.

Amesema kongomano hilo limekuwa wakati ni mwafaka waweze kujadili kwa pamoja namna moja ama nyingine ya kuzuia au watu kujitafakari kila mmoja kwa nafasi yake.
‘’Jamii, wazazi tuna wajibu wetu, vijana wana wajibu na serikali ina wajibu wake kufanya ili kupunguza hivi vitendo vya mmomonyoko wa maadili, tuwalee watoto wetu kwa kuwapa malezi yaliyo sahihi na tuwarithishe tamaduni zilizokuwa njema,’’amesema Ngonyani.
SOMA ZAIDI
Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo akiwemo, Christina Simo ameiomba jamii hasa wazazi kulea watoto katika misingi ya kimaadili ili waweze kuondokana na jamii yenye mmomonyoko wa maadili na wawe na taifa lililokuwa bora.
Mshiriki mwinginei ni Judith Chitanda kutoka Shirika lisilo la kiserikali la ‘Sauti ya Mwanamke’ mkoani humo ambaye ameitaja moja ya sababu inayopelekea uwepo wa tatizo hilo kwenye jamii ikiwemo matumizi ya simu kwa watoto pamoja na baadhi ya mitandao ya kijamii isiyozingatia maadili.
Kwa Upande wao Viongozi wa Dini akiwemo Askofu Yeriko Ngwema wa Dayosisi ya Kusini Mashariki Mtwara na Lindi (KKKT) alisema msingi bora wa familia unaanzia kwenye familia zao hivyo kama hautawekwa vizuri makuzi na ustawi wa watoto ambao ndiyo taifa la leo na kesho.



