Mgombea urais ukomo gharama bil 9/-

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema wagombea urais wamewekewa ukomo wa kutumia Sh bilioni tisa kugharamia uchaguzi.

Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika ofisi hiyo, Muhidin Mapejo amesema hayo Dar es Salaam wakati wa mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa.

“Kama unataka kwenda kufanya kampeni zako ukomo wako wa matumizi usivuke bilioni tisa (Shilingi). Kama wewe utakuwa na milioni 100 maana yake ni kwamba hata utakapokuwa unakwenda kwenye kampeni zingine, ukimpata mtu akachanga isivuke bilioni tisa,” alisema Mapejo.

Alisema kwa upande wa wagombea wa ubunge, ukomo kwenye majimbo umezingatia idadi ya watu, ukubwa wa majimbo, miundombinu ya majimbo hivyo kuna viwango tofauti na kiwango cha juu ni Sh milioni 136.

Mapejo alisema wagombea udiwani wamewekewa ukomo wa kutumia Sh milioni 16 kwenye kampeni zao. “Kama utaona kwamba mimi siwezi kufika milioni 16 labda nitakuwa na milioni tatu, milioni nne ama milioni tano hizo unaruhusiwa kutumia, cha msingi ulijaza fomu na fomu yako ilisema kwamba ni milioni 16,” alisema Mapejo.

Mkuu wa Sehemu ya Ruzuku, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Edmund Mugasha alisema miongoni mwa malengo ya sheria hiyo ni kutoa muongozo wa mchakato wa ndani wa Chama wa kuwapata wagombea.

“Mchakato wa ndani usimamiwe kisheria kwamba mtu asizidishe au asipatikane kiongozi mwenye pesa kupata uongozi na mwingine asiye na pesa akakosa uongozi,” alisema Mugasha.

Aliongeza: “Utaratibu umewekwa katika sheria hii, ni lazima ujaze fomu hizo zimeeleza nani anajaza na utaratibu gani wa kufuata”.

Mugasha alisema wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani wanatakiwa kufungua akaunti benki ambayo itaonesha matumizi yanayohusiana na uchaguzi.

“Mwanzoni chama peke yake kilikuwa kinaweka na kuwasilisha taarifa za benki kwa msajili (wa vyama vya siasa) lakini sasa kifungu cha 9 kinamtaka kila mgombea ambaye atakuwa ameteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi lazima awasilishe taarifa zake za kibenki kusaidia uwajibikaji,” alisema.

Mugasha alisema utaratibu huo utasaidia kudhibiti vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikiripotiwa katika kipindi cha uchaguzi.

Alisema sheria hiyo imempa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kupeleka pingamizi kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) iwapo itabainika mgombea au chama kimekwenda kinyume na sheria hiyo.

“Mtu huyu atakuwa anakosa sifa za kuteuliwa na tume ya taifa ya uchaguzi kwa sababu tu amekiuka taratibu, kwa hiyo msajili ana hiyo mamlaka kisheria,” alisema Mugasha.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button