Wanachama waeleza vigisu kura za maoni Chemba

DODOMA: SAKATA la uchaguzi wa kura za maoni nafasi ya ubunge limeshika kasi katika Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma baada ya wachanama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kueleza kuwa utaratibu wa upigaji kura na wanachama hicho uligubikwa na hila, mizengwe na fitina.

Miongoni mwa mizengwe hiyo  ni mawakala kufukuzwa katika chumba cha kuhesabu kura na kura kupigwa na watu ambao sio wanachama wa chama hicho.

Mmoja wa wana CCM, Buruhani Masare mkazi wa kata ya Chandama amesema alikuwa mmoja wakala wa mmoja wa wagombea ubunge wa Jimbo la Chemba, wapiga kura waliokuwa sio wanachama, wapiga kura walikuwa wakitumia kadi ya kupiga kura ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kinyume na utaratibu zilizowekwa na chama taifa.

Masare amesema mbali  ya hilo pia mawakala wa wagombea walifukuzwa nje muda wa kuhesabu kura hatua iliyolenga kutaka kumpitisha mgombea waliomlenga ambaye aliongoza upigaji kura katika Jimbo la Chemba hatua iliyoleta malalamiko katika zoezi zima la upigaji kura katika jimbo hilo lenye kata 26.

Amesema kutokana na hali hiyo wao kama wana CCM wamepeleka malalamiko katika ngazi za juu ikiwemo mkoa na taifa kueleza hali hiyo ya sitofahamu ya upigaji kura iliyogubikwa na changamoto nyingi za ukiukwaji wa makusudi wa viongozi wa chama ngazi ya kata na wilaya kwa masilahi yao.

‘’Tunaomba upigaji kura katika Jimbo la Chemba urudiwe kwa kuwa taratibu zima zilikiukwa kwa makusudi kikubwa upigaji kura ulipigwa na watu ambao si wana CCM,” amesema Masare.

Naye Said Selengema amesema upigaji wa kura za maoni katika Jimbo la Chemba haukuwa wa halali kwani viongozi wa chama walikuwa na mgombea wao waliomjengea mazingira mazuri ya kushinda katika upigaji kura.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Chemba,Moza Abdallah alipopigiwa simu na kuelezwa malalamiko ya wanachama wa jimbo hilo juu ya ukiukwaji wa taratibu na wapiga kura ambao sio wanachama,alisema kwa taratibu zote zilifuatwa na ikiwa ni pamoja na wapiga kura waliopiga kura walikuwa wanachama wa CCM  na mawakala waliofukuzwa katika chumba ni wale waliokuwa wameingia wakati wa upigaji kura na sio wakati wa kuhesabu kura kama taratibu zinavyoelekeza.

Amesema wagombea wakikosa ushindi huwa kuna malalamiko mengi na shutuma ambazo hazina msingi ili waonekane wanajitetea kwa wapambe wao au huwatumia wapambe kueneza uzushi kitu ambacho sio sahihi na kisema kura za maoni zilipigwa kihalali na waliopiga kura watu halali kwa mujibu wa taratibu za chama na sio vinginevyo.

Katika Jimbo la Chemba wagombea ubunge katika jimbo hilo walikuwa sita na kura zao kwenye mabano ni pamoja na Kunti Majala (5809),Juma Mkamia (1220), Amina Abdallah (784), Omari Futo (408),Khamis Mkotya (196) na Francis Julius (109) na majina  hayo kwa sasa yako katika vikao vya juu vya chama kwa uteuzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button