MCT, mawakili kulinda usalama wa wanahabari

ARUSHA: Baraza la Habari Tanzania (MCT) limezindua mpango maalum wa kushirikisha mawakili wa haki za binadamu ili kutoa msaada wa kisheria kwa waandishi wa habari, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Mpango huo umeanza rasmi jana jijini Arusha kwa mafunzo ya siku moja kwa mawakili 20 waliopatiwa uelewa kuhusu changamoto za kisheria zinazowakabili waandishi, hususan nyakati za uchaguzi.

Mafunzo hayo yaliyoongozwa na Jaji Mstaafu Robert Makaramba, yamegusia sheria zinazohusu vyombo vya habari ikiwemo Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na Sheria ya Makosa ya Mtandao.

Kwa mujibu wa MCT, mafunzo hayo yamewezesha mawakili kuongeza uwezo wa kutetea haki za kikatiba, kulinda uhuru wa uhariri na kusaidia michakato ya kidemokrasia. “Tunataka waandishi wafanye kazi kwa kujiamini, bila hofu ya vitisho au mashtaka yasiyo na msingi, wakijua kwamba kuna msaada wa kisheria utakaowalinda,” imesema sehemu ya taarifa ya Baraza hilo.

Takwimu za MCT zinaonesha kuwa licha ya kupungua kwa matukio ya ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari kutoka 119 mwaka 2018/19 hadi 18 mwaka 2022, bado changamoto zipo. Mwaka 2024 kulikuwa na matukio 27 ya ukiukwaji, na kati ya Januari hadi Agosti 2025 tayari matukio 17 yamerekodiwa, yakiwemo kukamatwa, vitisho, maonyo, utekaji nyara, na kuingiliwa kwa uhuru wa uhariri.

Huduma ya msaada wa kisheria kwa waandishi wa habari inatekelezwa kwa ufadhili wa International Media Support (IMS) na inatarajiwa kuendelea kwa siku mbili mfululizo jijini Arusha, kabla ya kuelekea Mwanza na Zanzibar. Aidha, MCT imetangaza kuwa waandishi watapatiwa nafasi ya kuzungumza na mawakili kwa faragha kuhusu masuala ya kisheria yanayowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kupitia mpango huu, MCT inaamini jitihada hizo zitachangia kuimarisha usalama wa waandishi na kuongeza weledi katika kuripoti masuala ya uchaguzi na jamii kwa ujumla.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button