Kodi mpya ya miti fursa kwa viwanda na ajira Iringa

IRINGA: Serikali imefanya marekebisho ya sheria ya kodi kwa bidhaa za miti zinazouzwa nje ya nchi, hatua ambayo inalenga kuhamasisha wamiliki wa viwanda kutumia mazao ya ndani kuzalisha bidhaa zilizokamilika hapa hapa nchini badala ya kuzipeleka nje.
Afisa Mwandamizi wa Kodi, Alex Mwambenja, amesema Sheria ya Kodi ya Mauzo ya Nje, Sura ya 196 ni moja ya sheria iliyofanyiwa mabadiliko ambayo sasa inataka kuwekwa ushuru wa mauzo ya nje wa asilimia 30 au Sh 150 kwa kilo moja, kutegemea kiwango kilicho juu zaidi, kwa bidhaa za mbao zilizolamishwa (veneered sheets).
Takwimu zinaonesha Mkoa wa Iringa ni moja ya maeneo makuu ya uzalishaji wa miti ya viwandani nchini, hususani aina za mipine na mikaratusi.
Kwa mujibu wa takwimu za Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), zaidi ya hekta 120,000 zimepandwa miti ya kibiashara katika mkoa wa Iringa, huku zaidi ya asilimia 60 ya miti yote inayozalishwa nchini ikipatikana Iringa na Njombe.
Bidhaa zinazotokana na miti hii ni pamoja na mbao, karatasi, nguzo za umeme, masanduku ya kuhifadhia bidhaa, plywood, na sasa veneered sheets ambazo zimeanza kusafirishwa nje.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya miti hiyo imekuwa ikisafirishwa ikiwa ghafi au ikiwa imeongezewa thamani kwa kiwango kidogo, jambo linalopunguza mapato kwa taifa.

Kwa ongezeko la kodi ya mauzo ya nje, mdau wa sekta hiyo, Tukuswiga Mwaisumbe alisema wamiliki wa mashamba ya miti na wafanyabiashara wahimizwe kuuza mazao hayo kwa viwanda vya ndani, hatua itakayochochea ujenzi wa viwanda vipya.
Alisema iwapo viwanda vya kuchakata miti vitapanuka mkoani Iringa, maelfu ya vijana wataajiriwa kuanzia ngazi ya ukataji, usafirishaji, uchakataji, hadi uuzaji wa bidhaa zilizoongezwa thamani.
Alisema, tafiti za Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) zinaonyesha kuwa kiwanda cha kati cha kuchakata mbao kinaweza kuajiri kati ya watu 150–300 moja kwa moja, huku mamia ya wengine wakinufaika kupitia ajira zisizo rasmi katika mnyororo wa thamani.
Naye Friday Simbaya alisema mbali na ajira, viwanda hivi vitachangia ongezeko la pato la taifa kupitia kodi, na wakati huohuo kuchochea maendeleo ya sekta nyingine zinazohusiana, ikiwemo ujenzi, samani, karatasi na bidhaa za nyumbani.
“Hatua ya serikali kuongeza kodi ya mauzo ya nje kwa bidhaa za miti inalenga kulinda viwanda vya ndani na kuhimiza kuongeza thamani ya mazao ya misitu kabla ya kusafirishwa,” alisema.
Ikiwa wenye viwanda na wawekezaji wataitumia fursa hiyo ipasavyo, alisema mkoa wa Iringa utabadilika zaidi na kuwa kitovu cha viwanda vya bidhaa za miti, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye ajira na pato la taifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa, Peter Jackson, alisema ni utaratibu wa kawaida kwa TRA kuwakutanisha wafanyabiashara na kuwapitisha kwenye mabadiliko ya kodi ili kuongeza uelewa.
Aliongeza kuwa walipa kodi wa mkoa wa Iringa wamekuwa mstari wa mbele kutimiza wajibu wao kwa hiari kwa kuwa wanajua sababu za kulipa kodi.



