Mhita ataka usimamizi bora maadili kwa watumishi

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita amewataka wajumbe wa kamati za Maadili na Maafisa wa Mahakama za Wilaya na Mkoa kuendelea kusimamia maadili ya Watumishi ili kuongeza uwazi na uwajibikaji wanapotekeleza majukumu yao.
Mhita amesema hayo jana kwenye mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wajumbe teule wa kamati za maadili na Maafisa wa Mahakama wa Wilaya na Mkoa yaliyotolewa na Tume ya Utumishi ya Mahakama baada ya kuapishwa na jaji Ruth Masam wa Mahakama kuu kanda Shinyanga kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda hiyo.

Mhita amesema misingi ambayo inatakiwa kuongoza kwenye kamati hizo ni viapo walivyopata na kuwa na maadili ambayo ndiyo inayotakiwa kufuatwa na bila maadili kuwepo nikushusha hadhi ya Mahakama.
“Mafunzo haya yana umuhimu mkubwa sana sababu yanatoa fursa kwa kuwajengea uwezo wajumbe hawa katika kutekeleza na kusimamia haki kwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi”alisema Mhita.
Mhita alitaka kuona kamati hizo zinaleta taswira chanya kwenye mahakama kwa wananchi na Kuongeza uwazi na uwadilifu kwa kutoa usawa na haki kwani wamekula viapo waende wakavifanyie kazi.
Naibu katibu anayeshugulikia Maadili kutoka Tume ya Utumishi wa Mahakama Alesia Mbuya amesema mafunzo kwa wajumbe hao imetokana na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 77 kifungu cha 36 cha sheria ya uendeshaji wa Mahakama namba nne ya mwaka 2011 ikieleza kuwepo Kamati za Maadili za Maafisa wa Wilaya na Mkoa.

Mbuya amesema yapo mafanikio yaliyopatikana ikiwemo kuongeza uelewa kwa watumishi wa Mahakama na kutekeleza majukumu ya msingi kama vile kuongeza kiwango cha uelewa kuhusu uwepo wa kamati za Maadili na Maafisa wa Mahakama za Wilaya na Mkoa.
Mbuya amesema Changamoto iliyokuwepo ni uelewa mdogo kwa baadhi ya wananchi na wadau kuhusu uwepo wa kamati za maadili na maafisa wa Mahakama katika ngazi za Mikoa na Wilaya pamoja na kutotambua majukumu yao.
“Kumekuwepo na baadhi ya kamati hizo kutotekeleza majukumu yao ipasavyo lakini mikakati iliyopo kwa Tume ya Mahakama ni kutoa elimu zaidi kwa wajumbe walioteuliwa na jamii wanao hudumiwa”amesema Mbuya.

Mbuya amesema Wajumbe wote wanatakiwa kuapa kabla ya kuanza kufanya kazi hilo ni takwa la kisheri na kupata mbinu bora kwaajili ya kusimamia watumishi wa Mahakama .
Kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Shinyanga Jaji Ruth Masam ambaye aliendesha zoezi la kuapisha wajumbe hao alieleza suala la msingi la kusimamia haki kwa wajumbe lazima lifuatwe bila kuangalia hali ya mtu.



