Serikali yawanyooshea vidole wanaoleta taharuki

SERIKALI imeonya vikundi, makundi ya watu pamoja na vyama vya siasa vitakavyoendesha kampeni za uchochezi, matumizi ya lugha za matusi na uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Imesisitiza kwamba Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi kupitia Jeshi la Polisi, wamejipanga kulinda amani ya nchi kwa gharama yoyote.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema hayo katika uzinduzi wa kituo cha polisi cha kisasa katika Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.
Aliwataka wananchi wawe huru kushiriki katika shughuli za kisiasa hususani katika kampeni zinazotarajiwa kuanza Agosti 28 na uchaguzi wenyewe utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huubila hofu yoyote kwani hali ya usalama wa nchi ni shwari.
Pamoja na kusisitiza kuwa hali ya usalama ni nzuri lakini bado aliwaomba wananchi kupuuzia taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya watu au vikundi vya watu kwa nia ya kuvuruga amani ya nchi.
“Pamoja na hali ya usalama nchini kuwa shwari kumekuwepo na baadhi ya Taasisi na watu binafsi au vikundi vya watu vinavyotoa taarifa kwa lengo la kuleta taharuki na hofu ya kiusalama nchini, nawaomba mzipuuze,” alisema.
Aidha, aliagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria wote watakaokaidi na kutaka kuvuruga amani na utulivu wa nchi.
Kadhalika alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutii sheria, kanuni na taratibu za nchi na kuwasisitiza wasikubali kujiingiza katika uhalifu wa aina yoyote katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Wakati huo huo, Bashungwa aliwashukuru na kuwapongeza wananchi wa wilaya hiyo kwa ushirikiano na kujitoa kwao kufanikisha mradi huo wa ujenzi wa kituo cha polisi cha kisasa kilichoanza kujengwa mwaka 2017 hadi kukamilika na kuzinduliwa rasmi.
“Suala la ulinzi na usalama linahitaji kuungwa mkono na watu wote kwa maana ni jukumu la watu wote, naomba tuondoe dhana kuwa jukumu hili ni kazi ya serikali peke yake, na kipekee naomba niwashukuru wananchi wa Chemba kwa kufanya hili kwa vitendo,” alisema.



