Tamasha la ‘Dream Car’ lapiga jeki fursa za kiuchumi Kilolo

IRINGA: Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amepongeza tamasha la ‘Dream Car’ lililofanya wilayani Kilolo hivi karibuni akilielezea kama mkakati wa kuhamasishana kimaendeleo, kuchochea ubunifu na kuwajengea vijana ari ya kuchapa kazi ili kufanikisha ndoto zao.
Katika uzinduzi huo, Kheri alisema tamasha hilo halikuwa burudani pekee bali ni daraja la kuonesha mafanikio, kujifunza kutoka kwa waliopiga hatua na kufungua milango ya uwekezaji mpya mkoani Iringa.
“Dream Car ni njia pia ya kuhamasisha vijana na wananchi kwa ujumla kutambua thamani ya kazi, bidii na mafanikio. Hii ni nafasi ya kuonesha tunapoweza kufika tukiamua kushirikiana,” alisema na kuongeza kwamba tamasha hilo limewapa deni ya tutakutana tena kuonesha mafanikio makubwa zaidi.

Aliongeza kuwa mkoa wa Iringa una fursa nyingi ambazo hazijatumika kikamilifu, ikiwemo Kilolo ambayo ni miongoni mwa wilaya tatu za mkoa huo.
Alizitaja fursa hizo kuwa ni kilimo, utalii, biashara na huduma mbalimbali.
“Kwa mfano mkoani Iringa, tunayo Hifadhi ya Taifa ya pili kwa ukubwa nchini, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, hali ya hewa ya kuvutia na mazingira salama ya biashara. Tunakaribisha wawekezaji kuchangamkia fursa hizi kwa ajili ya kujijengea kipato na kukuza uchumi wa mkoa wetu,” alisisitiza.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alisema serikali ya mkoa na wakurugenzi wa halmashauri wapo tayari kushirikiana na wabunifu wote ili kukuza mageuzi yenye tija, akisisitiza kuwa kila wazo jema litapewa nafasi ya kutekelezwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa tamasha hilo, Ramadhani Shemhilu, alisema lengo la Dream Car ni kufungua zaidi fursa za maendeleo wilyani Kilolo na mkoani Iringa na kuhamasisha wawekezaji wapya.
“Kwa Kupitia tamasha hili, tayari tumeona wawekezaji katika sekta ya biashara ya mafuta kuendeshea vyombo vya moto wakijitokeza. Hii ni ishara kuwa Kilolo inafunguka kimaendeleo,” alisema Shemhilu.

Alibainisha kuwa baada ya Kilolo, tamasha hilo litahamia wilaya nyingine mbili za Iringa na Mufindi, likiwa na lengo la kusambaza ari ya ubunifu na uwekezaji katika nyanja mbalimbali.
Mkoa wa Iringa umekuwa ukihamasisha wadau wa biashara na wawekezaji kutazama zaidi fursa mpya zinazopatikana, hususan katika sekta ambazo huduma zake bado ni chache, huku ukitazamwa kama lango la uchumi na sebule ya biashara kubwa nchini.
Mbali na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wengine waliodhamini tamasha hilo ni Puma Energy, Mix by Yas na IOP.



