Migiro: CCM itashinda kwa kishindo

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Asha-Rose Migiro ameripoti ofisini kwake jijini Dodoma.
Dk Migiro amesema ana imani CCM itashinda kwa kishindo kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu.
Alifika katika ofisi za CCM Makao Makuu (White House) jana jioni na kupokewa na Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake, Balozi Dk John Nchimbi, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mangella, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa na viongozi wa jumuiya za chama na wanachama.
Baada ya kuwasili, Dk Migiro alivalishwa vazi la kimila la Kabila la Wagogo na kukalishwa kwenye kiti huku akipewa jina na Mbeyu ikimaanisha ni mbegu bora.
Dk Migiro alisema umati wa wanaCCM waliompokea ni ishara kuwa chama hicho kitashinda kwa kishindo.
“Mahudhurio haya inaonesha kwamba tuko tayari kwa kuanza mapambano na kuhakikisha tunakipatia ushindi wa kishindo chama chetu…naishukuru sana imani mliyonionesha. Pamoja tutaongoza chama chetu kipenzi kufikia mafanikio katika uchaguzi ujao,” alisema.
Aliongeza: “Tunakwenda kuhakikisha ushindi kwa rais na mgombea mwenza wake, wabunge na madiwani tunapata ushindi mnono na nafasi zote tutaibuka kidedea. Katibu Mkuu (Dk Nchimbi) kama ni msitu ameufyeka na mimi nakuja kupita kwenye njia iliyonyooka nikiwa na wazee, vijana na wana CCM nikiwa na imani tutashinda na ushindi ni lazima”.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Nchimbi alisema uzoefu wa Dk Migiro ndani ya chama, serikalini na katika ngazi ya kimataifa unadhihirisha weledi wake na kuwajengea imani wanachama kuwa chama kipo mikono salama.
“Maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM Taifa (Rais Samia Suluhu Hassan) ya kukijenga na kuimarisha chama tumeyatekeleza na kufanya kwa mafanikio makubwa na wanaCCM wana imani kubwa na wewe (Dk Migiro),” alisema Nchimbi.