Dhamana ya vyombo vya habari wakati wa uchaguzi
KATIKA uchaguzi wowote duniani, vyombo vya habari vina dhima na mchango mkubwa wa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi zinazohusu uchaguzi kabla wakati na baada ya uchaguzi.
Kutokana na ukweli huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Nchini (TBC) anasema hata katika uchaguzi huu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 vyombo vya habari ni mhimili muhimu ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa uwazi, haki, utulivu na amani.
Dk Rioba anasema dhima ya vyombo vya habari ni kufuatilia yanayoendelea katika mchakato huu wa kuelekea uchaguzi, kusikiliza na kutoa taarifa kwenye jamii. “Lakini dhima nyingine ni kutoa elimu sasa hivi tunaelekea katika uchaguzi vyombo vya habari vinajukumu la kuwaita wataalamu mbalimbali ambao watajadili sera na masuala yanayohusu uchaguzi,” anasema.
Anaeleza kuwa: “Vyombo vya habari katika kipindi hiki cha uchaguzi, vinakuwa ni jukwaa kwa ajili ya mijadala na tumeona kuna mijadala kwenye vyombo mbalimbali vya habari hata sisi pale TBC tunakipindi cha mada kuu, lakini pia kutoa fursa kwa sauti za wanyonge kusikika na kusikilizwa.”
SOMA: Inec yazidi kunoa wanahabari Uchaguzi Mkuu
Anasema, “Vyombo vya habari vinajukumu pia la kuchambua ilani, ahadi za vyama na wagombea kufichua vitendo vya rushwa vinavyojitokeza kwa wagombea.”
Anaongeza kuwa vyombo vya habari vinaweza kuwa nyenzo ya ushawishi vikasaidia kutengeneza fikra za watu katika nchi wakajitazama kama watu vinaweza vikawa ni nyenzo ya kubadili tabia ndio maana huwa vinatumika kunapokuwa kuna kampeni ya namna fulani.
Dk Rioba anatudhihirishia kuwa endapo vyombo vya habari vikisambaza habari za kugawa wananchi zinaweza vikasababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi. Tumeona kwenye nchi mbalimbali za jirani zetu, namna vyombo vya habari vilivyotumika kushawishi wananchi kujitokeza kufanya maandamano na kuvuruga amani ya nchi hizo kipindi cha uchaguzi.
Kulingana na maoni ya Wachambuzi wa masuala ya siasa wanatukumbusha kwenye chaguzi zilizopita vyombo vya habari vilivyosaidia kuhakikisha uchaguzi unakamilika kwa amani na utulivu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Dk Kanaeli Kaale anasema waandishi wa habari na wachambuzi wanamchango mkubwa kwa sababu wanapokuwa wanazungumza wanapitia kwenye vyombo vya habari wanaaminiwa kwa ukubwa zaidi.
“Vyombo vya habari ndio daraja kati ya serikali na wananchi kwa hiyo kupitia ule uchambuzi wananchi wanapata ile elimu ya upigaji kura na mambo muhimu ya kuzingatia na ya kuyapuuza,” anasema Dk Kaale.
Anasema, “Kwa sababu mwananchi anaeenda kupiga kura lazima awe na elimu sahihi ajue amchague nani kwa hiyo wachambuzi wanavyochambua wanatoa elimu kwa umma ili kila mtu anapoenda kupiga kura ajue anamchagua nani.”
Anaongeza kuwa: “Kwa hiyo wachambuzi wale wa kimataifa na ndani wanamchango mkubwa sana kwenye kuelimisha, kukosoa na kuelimisha wananchi.” Kwa upande wake Mchambuzi wa siasa na Mwangalizi wa nje wa uchaguzi, Nixon Katembo anasema anakiri kuwa vyombo vya habari vinamchango mkubwa wa kudumisha amani.
“Kuzingatia misingi bora ya uandishi wa habari na kutoa msimamo inayolenga kuleta amani na maendeleo na mshikamano ndani ya jamii na pia kuliendeleza Taifa la Watanzania kisiasa na Uchumi,” alisema. Mdau wa masuala ya Uchaguzi kutoka kata ya Kipunguni, Elisha Marijani anasema vyombo vya habari vinaweza viharibu amani ya sehemu husika endapo vikitumika vibaya.
“Ni mashahidi tumeona ripoti nyingi kutoka kwa nchi jirani zetu zilivyoweza kuchochea machafuko kwenye nchi za wenzetu wakati wa uchaguzi,” anasema Marijani.
Anaeleza, “Tumeona nchini Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na nchi nyinginezo namna wananchi wanavyofanya mambo yanayoleta machafuko lakini yote hayo msingi mkubwa wa hayo ni vyombo vya habari badala kutumika kuzuia vinatumika vinachochea kwa kiasi kikubwa kutokea machafuko hayo.”
Anaongeza kuwa: “Pale panapokuwa pametokea vurugu kutoka Chama cha Siasa A na B, vyombo vya Dhamana ya vyombo vya habari wakati wa uchaguzi habari vinatakiwa kutumia busara kutosambaza yale mabaya yaliyotokea kwenye machafuko hayo ili kuepusha uchochezi na uvunjifu wa amani.
Anaeleza kuwa: “Kwenye chaguzi zilizopita mamlaka zinazosimamia vyombo vya habari zilijitahidi kuvidhibiti kutotoa habari zenye muelekeo wa uvunjifu wa amani na ndicho kilichotusaidia kumaliza chaguzi zile kwa amani na utulivu.”
Anasema katika uchaguzi wa mwaka huu Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), ijitahidi kusimamia kikamilifu maadili ya vyombo vya habari na kuwapa semina na maelekezo ya nini wanatakiwa wafanye na nini hawatakiwi kufanya.
“Ninadhani, JAB imeanza kutekeleza majukumu yao hivi karibuni kwenye chaguzi zilizopita majukumu ya waandishi wa habari na usimamizi wa vyombo vya habari yalikuwa yanasimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), lakini sasa ninaamini JAB na TCRA wakishirikiana hakuna kitakachoharibika nchini,” anaeleza.
Ni Dhahiri, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa habari kwa kushirikiana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mamlaka ya mawasiliano (TCRA) wameshaweka mikakati ya kuwasimamia ipasavyo wanahabari.
Tumeona wameanza kutoa vitambulisho vinavyomtambua mwanahabari anayetakiwa kufanyakazi ya taaluma hiyo na kuonyesha msimamo wake wa kuwadhibiti wanahabari ambao hawajasomea taaluma hiyo ili kuepusha kila mtu kurusha taarifa za uchaguzi wakati hana taaluma ya uandishi na hajui miiko yake.
Kwa kudhibiti hilo la kila mtu kurusha maudhui ya uchaguzi INEC imejipanga kutoa vitambulisho kwa waandishi wa habari wote, watakaotaka kuandika habari za uchaguzi siku yenyewe ya uchaguzi ili kuepuka kusambaa kwa taarifa za uzushi zenye lengo la kuleta machafuko nchini.
Uchaguzi mkuu wa Mwaka huu wa saba tangu Tanzania iingie kwenye mfumo vya vyama vingi. Uchaguzi wa kwanza ulifanyika mwaka 1995, ukifuatiwa na wa mwaka 2000, 2005, 2010, 2015 na 2020 na chaguzi zote zilikamilika nchi ikiwa na amani na utulivu.



