Geita kuupokea Mwenge September Mosi

GEITA: MKOA wa Geita unatarajia kupokea Mwenge wa Uhuru Jumatatu ya Septemba 01, 2025 katika kijiji cha Rwezera ukitokea Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella ametoa taarifa hiyo Agosti 30, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.
Shigella amesema kwa mwaka 2025 Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani Geita unatarajia kupita na kukimbizwa katika jumla ya miradi 61 yenye thamani ya sh bilioni 164.4.
Amesema mwaka 2024 mwenge wa Uhuru ulikimbizwa ndani ya mkoa wa Geita na kuweza kufikia miradi 65 yenye jumla ya thamani ya Sh bilioni 32.2.
“Kuna ongezeko kubwa sana hadi Sh bilioni 164.4 kutoka miradi ya Sh bilioni 32.2 mwaka 2024, hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 80
“Hii ni kutokana na ukweli kwamba serikali ya awamu ya sita imeongeza usimamizi wa makusanyo ya mapato kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali”, amesema.
Amesema miradi inayoendelea kutambuliwa na mwenge wa uhuru kila mwaka inatokana na kazi kubwa iliyofanyika chini ya serikali ya awamu ya sita pamoja na mwitikio wananchi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo.
“Pia wapo wadau na taasisi binafsi ambao wanatambua na kuunga mkono juhudi za maendeleo inayotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa”, amesema Shigella
Shigella ametumia nafasi hiyo kuwaomba na kuwasihi wananchi wa mkoa wa Geita kujitokeza kwa uwingi katika mapokezi na mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2025.



