Dk Nchimbi: CCM pekee inaweza kuleta maendeleo

MGOMBEA Mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema chama hicho pekee kina uwezo wa kuiwezesha Tanzania kupata maendeleo.
Dk Nchimbi alisema hayo alipohutubia mamia ya wananchi wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara juzi.
Alisema wingi wa watu waliojitokeza kwenye mkutano huo ni ishara ya ushindi mkubwa unaotokana na kuthamini kazi zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika miaka minne ya kuiongoza Serikali ya Awamu ya Sita.
Dk Nchimbi alisema CCM pekee inaweza kutoa ahadi na kuzitekeleza kwa vitendo na Ushahidi, kwamba hata vyama vingine vya siasa vinalijua hilo.
Alitaja mafanikio yaliyopatikana Rorya ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia ni kujengwa hospitali mpya ya wilaya, ongezeko la zahanati kutoka 31 hadi 40, vituo vya mama na mtoto kutoka vitatu hadi vitano na kuongezeka kwa watumishi wa afya kutoka 292 hadi 402.
Pia, alisema shule za msingi zimeongezeka kutoka 137 hadi 152, sekondari kutoka 39 hadi 49 na miradi ya maji iliyogharimu zaidi ya Sh bilioni 9.7 imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
“Kwa sasa vijiji vyote 87 vya Rorya vimepata umeme na vitongoji 279 kati ya 508 vimeunganishwa. Vile vile, mabwawa ya ufugaji wa samaki yameongezeka kutoka 21 hadi 48 na vizimba kutoka 32 hadi 149. Hii yote ni kazi ya CCM na uongozi wa Rais Samia,” alisema Dk Nchimbi.
Alisema kupitia Ilani ya CCM 2025-2030 chama hicho kinaahidi kujenga zahanati mpya 10 na vituo vya afya vya kisasa vitano, kuongeza watumishi 150 katika sekta ya afya, kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Veta, kujenga shule mpya za sekondari 10 na shule za msingi tano.
Vile vile, Dk Nchimbi alisema CCM itahakikisha vitongoji vyote 279 vya Rorya vinapata umeme, asilimia 95 ya wananchi wanapata maji safi na salama, kujengwa majosho mapya 19, kuanzishwa ranchi tatu ndogo za mifugo, kuongeza vizimba vya samaki kutoka 149 hadi 300 na mabwawa kutoka 48 hadi 100.
“Wananchi wa Rorya niambieni, chama gani kingine kitaweza kufanya haya? Hakuna. Ni CCM pekee inayotekeleza na kuahidi mambo yanayotekelezeka. Ndiyo maana tunasema kwa kujiamini kuwa ushindi wetu ni wa uhakika,” alisema Dk Nchimbi.