Mgombea kuomba kura kwa Whatsapp, TikTok, Facebook

MBEYA; MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Uyole jijini Mbeya kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Ipyana Njiku amesema atafanya kampeni zake kidijiti.
Njiku alisema atatumia mitandao ya kijamii ikiwemo ya WhatsApp, TikTok na Facebook kwa sababu wapiga kura wengi sasa wanatumia majukwaa hayo kupata habari na mawasiliano.
Aliieleza HabariLEO kuwa atatumia mtandao wa Facebook kwa kulipia vifurushi vya matangazo ili kusambaza sera kwa watumiaji wa mtandao huo waliopo ndani ya Jimbo la Uyole.
“Kila wiki nitakuwa nalipia sera moja na wiki inayofuata nitajikita kwenye kipaumbele kingine, hii ni njia rahisi na ya kisasa kuliko kufanya mikutano ya hadhara ambayo inahitaji rasilimali kubwa,” alisema Njiku jana.
Pia, alisema atapita mitaani akitumia kipaza sauti kuwaeleza wananchi sera na mikakati yake ya kuwaletea maendeleo.
Njiku alisema kampeni za kidijiti zinaweza kuwa na ufanisi sawa na mikutano ya hadhara, hivyo ana matumaini wapigakura watavutiwa na mfumo wake na kusaidia kusambaza taarifa zake kwa wengine.
Alisema endapo atachaguliwa atajenga soko la kisasa mfano wa Soko la Kisutu kwa ajili ya wajasiriamali, kujenga kituo cha mabasi ya kisasa na kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo la maji kwa kuyaleta kutoka Ziwa Nyasa hadi Jimbo la Uyole.
Alitaja vipaumbele vingine ni kuboresha barabara za mitaani, kujenga viwanja vya kisasa vya michezo, kugawa kompyuta mpakato kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na kutoa simu aina ya iPhone kwa kila mwalimu ili kuhimiza matumizi ya teknolojia shuleni.
Njiku pia aliahidi kuweka huduma ya intaneti bure katika ofisi za walimu na maeneo ya mikusanyiko ya kijamii yakiwemo masoko na vituo vya mabasi.



