Akili unde isichafue pambazuko la wanawake kuchaguliwa 2025

MWAKA 2025 kumepambazuka kwa wanawake kuchanua katika siasa na uongozi na ndio maana ‘Kura Yako ni Haki Yako Jitokee Kupiga Kura’ Oktoba 29, 2025 kuchagua maendeleo bila kujali kiongozi mleta maendeleo ni mwanamke au ni mwanaume.

Ni mwaka wa mapambazuko na wanawake kuchanua katika uchaguzi na uongozi wa kisiasa kwa kuwa tofauti na awali, mwaka huu wanawake wamejitoa katika minyororo na mahandaki ya mfumo dume unaowafanya waogope kupambania nafasi mbalimbali, badala yake sasa wamejitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi kwa kushindana katika majukwaa.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, wanawake watatu wamejitokeza na kuchukua fomu katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hao, ni Rais Samia Suluhu Hassan wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayetetea nafasi yake, Mwajuma Mirambo wa chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD) na Swaumu Rashid kutoka chama cha siasa cha United Democratic Party (UDP).

Hongera wanawake wa Tanzania maana Tanzania itajengwa na Watanzania na si wanaume au wanawake pekee. Kinachoonesha kuwa 2025 ni mwaka wa pambazuko kwa wanawake katika uongozi wa kisiasa ni idadi ya wanawake wengi waliojitokeza na vyama vyao kupitisha kumi kuwa wagombea wenza ili ambaye chama chake kitapata ushindi, basi awe makamu wa rais.

Wanawake hao ni Mashavu Alawi Haji wa UMD, Amana Suleiman Mzee wa Tanzania Labour Party (TLP), Azza Haji Seleiman wa Chama cha Demokrasia Makini na Chausiku Khatib Mohammed wa chama cha National Legue for Domocracy (NLD).

Wengine ni Eveline Wilbard Munisi wa NCCR- Mageuzi, Satia Mussa Bebwa wa SAU, Fatma Abdullahbib Fereji wa ACT- Wazalendo, Chumu Juma wa AAFP, Husna Mohamed wa Chama cha Wananchi (CUF) na Devota Minja wa CHAUMA. Mlango wa matumaini ulifunguliwa na Anna Senkoro, mwanamke wa kwanza kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 kupitia chama cha PPT- Maendeleo.

Akiwa mgombea pekee wa kike, alishika nafasi ya nane kati ya wagombea 10 na kuweka historia. Mwaka 2015, Queen Sendiga wa ADC na Anna Mghwira (ACT-Wazalendo) walikuwa wanawake pekee waliojitosa kuwania urais.

Samia alipeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya Mgombea Mwenza huku John Magufuli akiwania na kushinda katika kinyang’anyiro hicho na Rais wa Tanzania huku Samia akiwa Makamu wa Rais. Rais Samia aliingia madarakani Machi 19, 2021 kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na kifo cha mtangulizi wake Magufuli Machi 17, 2021.

Upepo wa kisiasa nchini umebadilika kwani katika miaka ya nyuma ‘zilivaa joho’ la ujinsia zikitawaliwa na wanaume hasa kwa nafasi za urais na umakamu wa rais. Upepo umebadilika kwa kasi inayoleta tumaini jema. Mawimbi ya siasa za ujinsia yametoweka kwa kasi baada ya utendaji wa Samia kuthibitishia Watanzania kuwa kama ilivyo kwamba wapo wanaume wengi wasioweza uongozi, ndivyo ilivyo kwamba wapo wanawake wengi wanaoweza uongozi.

Hii inatokana na uongozi bora aliouonesha katika kipindi alichokuwa madarakani kwa mtindo wa ‘maneno kidogo, vitendo kwa wingi.’ Ndio maana Uongozi wa Samia umekuwa mwanga wa wanawake katika uchaguzi 2025.

Licha ya mafanikio hayo, maendeleo ya sayansi na teknolojia hayajawahi kuja na mafanikio pekee bila changamoto au hatari kama ilivyo sasa ambapo kuna maendeleo hayo katika uwanja wa demokrasia nchini, lakini kuna ‘kidudu-mtu’ kiitwacho ‘Akili Unde’ wengi wamezoea kukiita ‘AI’ ambayo ni kifupi cha ‘Artificial Intelligence.’

Kwa siku na miezi ya karibuni, INEC na taasisi mbalimbali zimeweka nguvu kubwa kuelimisha umma mintarafu umakini zaidi dhidi ya uwepo wa matumizi ya akili unde hususani katika kipindi cha uchaguzi kwani kuna hatari ya ongezeko la kasi ya kusambaa kwa taarifa za uongo, chuki, matusi, udhalilishaji na uchochezi mitandaoni.

Kwa mfano, Agosti 18, 2025 wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) walikutana Dar es Salaam kujadili masuala mbalimbali likiwamo la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025 na matumizi ya akili unde.

Wasilisho kuhusu suala hilo lilifanywa na Katibu Mkuu wa Kwanza wa Jumuiya ya Kimataifa ya Viongozi Wanawake (WPL), Neema Lugangira. WPL (Women Political Leaders) inahusisha marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu, mawaziri, wabunge na mameya.

Anasema: “Kikanda, niliteuliwa na Jumuiya ya Tume za Uchaguzi Afrika (Association of African Election Authorities – AAEA) kuwa Mjumbe wa Kikosi Kazi kilichopewa jukumu la kuandaa Mwongozo wa Matumizi ya Mitandao ya Kijamii na Teknolojia katika Uchaguzi Afrika na kimataifa, nilikuwa mwandishi mwenza wa Azimio la Bunge la Dunia (IPU) kuhusu Akili Unde lililolenga kuangazia athari za akili unde (AI) katika demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.”

Kwa mujibu wa Lugangira, mwaka 2023, AAEA ilipitisha mwongozo muhimu kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii na teknolojia katika uchaguzi. Mwongozo huo ulilenga kulinda uhalali wa uchaguzi kwa kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki pamoja na kukabiliana na habari potofu na propaganda hususani zinazoenezwa kupitia akili unde na mitandao ya kijamii.

Anasema licha ya faida zake, akili unde inaweza kutumiwa vibaya kutangaza maudhui na maoni yaliyopandikizwa ili kuharibu heshima ya mgombea hususani wanawake kwa mashambulizi ya matusi na ukatili wa kijinsia mtandaoni.

Katika mkutano huo, Lugangira pia amekabidhi nakala 40 za Mwongozo wa Jumuiya ya Tume za Uchaguzi Barani Afrika kuhusu Matumizi ya Mitandao ya Kijamii na Teknolojia kwenye Chaguzi za Afrika na nakala 20 kwa Murugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dk Rose Reuben na Mwenyekiti Mstaafu wa Tamwa, Joyce Shebe.

Anasema: “Vyombo vya habari ni mshirika mkubwa kulinda uchaguzi dhidi ya matumizi mabaya ya teknolojia. Kwa kushirikiana, tunaweza kuhakikisha uchaguzi wetu ni wa haki, salama, na unaowapa nafasi sawa wanawake na wanaume.” Kwa nyakati na mafunzo mbalimbali kwa wanahabari makao makuu ya Tamwa Dar es Salaam, Dk Rose wa Tamwa amekuwa akihimiza waandishi wa habari kuwa makini na namna ya utumiaji wa akili unde katika kipindi cha uchaguzi kwa kuchuja taarifa wanazopokea kabla ya kuzisambaza au kuzifanyia kazi.

Hii ni kusema kuwa matumizi mabaya ya AI yasiachwe kuwa fimbo ya kuchapa na kushona midomo huku yakifunga miguu na mikono ya wanawake wasishiriki kikamilifu katika kampeni za kisiasa hususani wanaogombea pamoja na kujitokeza kupiga kura kutokana na vitisho na taarifa au maudhui ya uongo.

Ikumbukwe kuwa, kadiri nafasi ya wanawake inavyokuwa kubwa katika kampeni, ndivyo uwezekano wa kampeni unavyozidi kutumia mbinu zisizo za ukatili, hata katika mazingira yanayokandamiza sana. Katika warsha ya Julai 17, 18, 2025 iliyoandaliwa na TAMWA, kwa kushirikiana na Global Action for Peacebuilding (GAPI) kwa ufadhili wa GIZ, Njokii Kariuki kutoka GAPI Nairobi, Kenya anasema zipo taarifa zinazotengenezwa makusudi kushawishi hisia za watu au kuharibu sifa za watu au taasisi, hasa katika kipindi cha uchaguzi hivyo umakini kwa kila mtu unahitajika.

“Kuna maneno yanaandikwa kwa makusudi ya kuleta taharuki au kuchochea hisia za chuki. Waandishi wanapaswa kuwa waangalifu, kufanya uchunguzi wa kina. Kabla ya kuchapisha taarifa yoyote, lazima ujiulize, nani alisema? Lini? Kwa muktadha upi? Na kwa lengo gani?” kwa kuwa baadhi ya taarifa hutolewa kwa kutumia muktadha wa zamani na kuwasilishwa kama matukio ya sasa hivyo kupotosha umma na kuibua mgawanyiko.”

Ndio maana Kisemeo cha Wanyonge kinasema: “Akili unde isichafue pambazuko la wanawake kuchanua katika Uchaguzi Mkuu 2025.” SOMA:Wanahabari waagizwa kulinda taarifa binafsi

Habari Zifananazo

One Comment

  1. I make $88 an hour to work part time on a laptop. I never thought it was possible but my closest friend easily made $18,000 in 3 weeks with this top offer and she delighted me to join. .Visit the following article for new information on how to access…….
    .
    HERE——————————————⊃⫸ http://Www.Cash43.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button