Uzalendo utawale wakati wa kuripoti Uchaguzi Mkuu

AMANI, utulivu, umoja na mshikamano ni vitu muhimu ambavyo nchi ya Tanzania imebarikiwa na vinaliliwa na kutafutwa na mataifa mengine.
Amani iliyopo ni chanzo cha shughuli za kiuchumi, kulea na kukuza vizazi vyenye afya bora kutokana na kukua kwa utulivu, kichocheo cha elimu bora na maendeleo mengine ya nchi. Kuwa na demokrasia ni moja ya sababu za amani na utulivu uliopo nchini zinazowezesha kufanyika uchaguzi ambao ni sehemu ya utekelezaji wa demokrasia.
Tumeshuhudia katika baadhi ya nchi vyombo vya habari vimetumika kama nyenzo ya uvunjifu wa amani kutokana na namna wanavyoripoti matukio wakati wa uchaguzi kuchochea vurugu na migogoro inayosababisha vifo, uharibifu wa mali na uvunjifu wa amani.
Kwa kulitambua hilo waandishi wa habari wa ndani na nje wanapaswa kutumia kalamu zao vizuri wakati wa kuripoti Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Mwaka 2025 kwani kalamu zao ni nyenzo muhimu kudumisha au kuvuga amani iliyopo nchini.
Katika mafunzo ya waandishi wa habari yaliyofanyika Agosti 21, 2025, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi aliwaagiza waandishi wa habari waandike habari za Uchaguzi Mkuu wakizingatia uzalendo badala ya masilahi binafsi.
Profesa Kabudi aliwasisitiza waandishi waandike habari za uchaguzi zenye masilahi ya taifa na wajiepushe na vitendo vya rushwa kwa kutumia vyombo vyao kujenga mambo yenye tija kwa umma, kwa kueleza sera za vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi na si kuandika habari za uchochezi.
“Watanzania watangulize uzalendo mbele, hatuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania, tuhakikishe uchaguzi unakuwa wa amani na wanahabari zingatieni misingi ya taaluma; kuweni wazalendo, uchaguzi uwe wa amani,” alisema.
Kauli ya Profesa Kabudi inatukumbusha kuwa uzalendo ni kiungo muhimu katika uchaguzi huu hivyo waandishi wa habari wazawa lazima wawe wazalendo kuilinda nchi. SOMA: Kabudi: Tuithibitishie dunia utulivu Tanzania
Uzalendo ni pamoja na waandishi kuepuka kuandika taarifa zenye uchochezi. Ili kuepuka kufanya uchochezi waandishi wa habari wanapaswa kuzingatia na kujua viashiria vya migogoro vikiwemo vitisho na manyanyaso.