Mradi wa visima majimboni wafika 85% Nyang’hwale

GEITA: WAKALA wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Nyang’hwale imefikia asilimia 85 ya utekelezaji wa mradi wa visima majimboni wenye lengo la kuchimba visima maalum vya kupunguza adha ya maji.

Ruwasa wilayani Nyang’hwale inatekeleza mradi wa maji wa visima vitano vya jimbo katika vijiji vitano ambavyo ni Kanegele, Mwingiro, Shabaka, Wavu na Lubando na kuongeza upatikanaji wa maji kufikia asilimia 77.4.

Kaimu Meneja wa Ruwasa wilayani humo, Suzana Gogadi ametoa taarifa hiyo Septemba 03, 2025 kwa viongozi wa mbio za mwange kitaifa 2025 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi wa visima vitano iliyofanyika kijiji Shabaka.


“Wananchi takribani 5,000 waishio katika vijiji hivyo watapata huduma ya maji safi na salama hivyo kupunguza magonjwa ya milipuko”, amesema Suzana.

Amesema vyanzo vya maji katika mradi ni visima virefu vitano vyenye uwezo wa kutoa jumla ya lita 21,150 kwa saa ambapo mkataba wa ujenzi ulianza Januari 06, 2025 na unatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2025.

Amesema mradi huo unatekelezwa kwa mfumo wa Force Account na kwa kutumia mafundi wa ndani (local fundi) ambapo gharama za utekelezaji mradi wa maji katika Vijiji hivi vitano ni sh milioni 327.

“Hadi sasa Jumla ya kiasi cha shilingi milioni 137.15 kimekwisha lipwa kwa ajili ya shughuli ya ufungaji wa Sola, pampu, ununuzi wa matenki na malipo ya Local Fundi.

“Chanzo cha fedha za mradi huu ni kupitia Mpango wa Malipo kulingana na Matokeo (PforR) na Fedha Maalum (Special Fund)”, amesema Suzana.

Amesema mradi unahusisha ufungaji wa mfumo wa sola na pampu, Ujenzi wa Vioski, kuweka mfumo wa maji na tenki la plastiki lenye ujazo wa lita 10,000, Uchimbaji na ufukiaji wa mitaro ya bomba yenye urefu wa mita 9,467.

Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame amekiri kuwa uchimbaji wa visima virefu majimboni ni msaada mkubwa katika kuboresha huduma ya maji safi na salama.

Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2025, Isimail Alli Ussi amesema mradi visima majimboni ni juhudi za serikali kukabili tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama hivo usimamizi thabiti unahitajika kufikia malengo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button