Zuchu aitafuta bilioni moja

MSANII nyota wa Bongo Fleva, Zuhura Othman “Zuchu”, anaendelea kuandika historia katika muziki wa Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa takwimu za leo(Agosti 27, 2025), chaneli yake rasmi ya YouTube imefikia watazamaji zaidi ya milioni 909, hatua chache tu kuelekea rekodi kubwa ya kufikisha bilioni moja.
Hii ni hatua adimu kwa msanii wa kike katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikithibitisha ubunifu wake, kazi ngumu na mapenzi makubwa kutoka kwa mashabiki wake duniani.
Zuchu si mgeni kwenye rekodi mwaka 2023 alitambulika kama msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufikisha watazamaji milioni 500 kwenye YouTube. Safari yake ya sasa kuelekea bilioni moja ni ushahidi kuwa jina lake linaendelea kung’aa, na historia zaidi zipo njiani.
Kinachovutia zaidi ni upeo wa muziki wake unaovuka vizazi; nyimbo zake zinaenziwa na watoto, vijana, na hata watu wazima, jambo linalomfanya awe daraja la muziki kwa rika zote.
Swali kwa mashabiki: Unadhani Zuchu afanye nini ili azidi kuchachambua kimataifa na kuvunja rekodi zaidi?



