Mradi wa maji wa bil 2/- wakamilika Mbogwe

GEITA: WAKALA wa Maji na Usafi Mazingira vijijini (RUWASA) wilayani Mbogwe imekamilisha mradi mkubwa wa maji uliopo katika eneo la Ushirika-Mlale ambao ulianza kujengwa Aprili 2024 hadi Aprili 2025.
Fedha za mradi huo zimetokana na mfuko wa PforR huku Mkandarasi wa mradi ni Otonde Construction & General Supplies Limited kutoka Mwanza kwa gharama ya Sh bilioni 2,04 pamoja na VAT na amelipwa sh bilioni 1.84.
Meneja wa RUWASA wilaya ya Mbogwe, Mhandisi Rodrick Mbepera ametoa taarifa hiyo mbele ya viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 walipowasili kwa ajili ya kulagua na kuzindua mradi huo.

Amesema mradi huo mkubwa wa maji utanufaisha wananchi takribani 21,009 wa vijiji sita vya Ikobe, Isebya, Ushirika, Mlale, Kadoke na Ushetu ambapo kabla ya mradi kukamilika walikuwa wanatumia maji yasiyo salama.
Mhandisi Rodrick amesema chanzo cha maji katika mradi huo ni visima virefu vya wastani wa mita 84 vyenye uwezo wa kutoa lita 20,300 kwa saa na vinavyotumia umeme.
Amesema kabla ya uzinduzi mradi huo uliwekewa jiwe la msingi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2024 Godfrey Eliakimu Mnzava.
“RUWASA imejenga mtandao wa mabomba wa km 50.059, matenki 3 ya ujazo wa lita 150,000, 75,000 na 50,000 juu ya minara ya mita 9, 9 na 12, nyumba za mitambo 3 na vituo vya kuchotea maji 35 vyenye dira za malipo ya kabla.
“Mradi umetekelezwa kwa lengo la kufikisha huduma ya maji safi karibu na makazi yao na unasimamiwa na CBWSO ya Imalabupina Nanda”, amesema Mhandisi Rodrick.

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi amepongeza ukamilishaji wa mradi huo na kuwataka wananchi kutumia maji safi na salama na kuachana na matumizi ya maji yasiyo salama kwa mazoea.
Ussi ameitaka RUWASA kuongeza uwajibikaji kufanikisha azima ya serikali kuendeleza kutoa huduma bora ya maji ambayo ni moja ya huduma muhimu kwa maendeleo endelevu.



