Sh bilioni 3.49 kukamilisha jengo la utawala Bukombe

GEITA: SERIKALI imepanga kutumia kiasi cha Sh bilioni 3.49 kukamilisha Mradi wa Jengo la Utawala katika Halmashauri ya wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Mradi huo unatekelezwa katika kitongoji cha Bomani kata ya Katente tarafa ya Ushirombo wilayani humo kwa sasa umefikia asilimia 53 ya utekelezaji.
Mhandisi Msimamizi wa mradi, Mhandisi Jackson Mugiye ameeleza hayo kwa viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 katika uwekaji wa jiwe la msingi.
Mhandisi Jackson amesema Mradi ulianza Machi 04, 2024 na unatarajiwa kukamilika Januari 04, 2026 kwa mjibu wa mkataba ambao mkandarasi alisaini na halmashauri.
Amesema mpaka jumla ya Sh milioni 985.1 zimekwishalipwa kati yake malipo ya awali ni kiasi cha Sh milioni 444.6, malipo ya kwanza Sh milioni 306.9, malipo ya pili ni Sh milioni 233.58.

“Mradi unatarajiwa kurahisisha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi ndani ya eneo moja kufuatia ofisi zote kuwepo ndani ya jingo moja”, amesema Mhandisi Jackson.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi amesema kuwa hatua hiyo ni mwendelezo wa serikali kuhakikisha inaweka mazingira bora ya utendaji, utumishi na uwajibikaji.
“Ussi aliitaka halmashauri kuimarisha usimamizi wa mradi huo na kufuatilia kwa ukatibu ili kuhakikisha mpango kazi wa mradi unafuatwa na mkandarasi anayetekeleza mradi huo”, amesema.
Amesema baada ya ukaguzi wa kina wa mradi huo viongozi wa mbio za mwenge wameridhika na maendeleo lakini kuna maelekezo ambayo yametolewa kukamilisha mradi kwa ufasaha.



