Jasmine Ng’umbi: Dk Samia chaguo la vijana

IRINGA: Mteule wa ubunge kupitia nafasi ya vijana kutoka Wilaya ya Mufindi, Jasmine Ng’umbi, ameibua nguvu mpya katika siasa za Mkoa wa Iringa baada ya kumshukuru kwa heshima na upendo Rais na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaamini vijana na kuwapa nafasi ya uongozi ndani ya chama na serikali.

Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi na wanachama wa CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika leo Septemba 6, 2025, mjini Mafinga, Jasmine alisema uteuzi wake si ushindi binafsi, bali ni ushahidi tosha wa dhamira ya Rais Dk Samia kuwainua vijana.

“Nilikuwa namba saba kwenye orodha ya wagombea, lakini nikapandishwa hadi nafasi ya sita. Hii si heshima kwangu peke yangu bali kwa vijana wote wa Mufindi na Tanzania nzima. DK Samia ni chaguo la vijana na chaguo la maendeleo,” alisema kwa msisitizo huku akishangiliwa kwa nguvu.

Katika tukio lililowagusa wengi, Jasmine alipiga goti hadharani na kumshukuru Rais Dk Samia, akiapa kuwa ifikapo Oktoba 29 atahakikisha kura za wananchi wa Mufindi na Iringa zinampeleka mgombea huyo wa CCM Ikulu kwa kishindo.

Akaongeza kwa kujiamini: “Vijana wa Mufindi tumejiandaa kuwa jeshi la kampeni la Samia. Tutapita kila kijiji, kila kata na kila mtaa kuhakikisha Rais wetu anashinda kwa kishindo cha historia.”

Alisisitiza kuwa uteuzi wa vijana wengine akiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, ni ushahidi kwamba Dk Samia ameamua kwa dhati kulipa taifa nguvu mpya ya kisiasa kupitia vijana.

Mkutano huo uligeuka kuwa tamasha la kisiasa baada ya wafuasi wa CCM kushangilia bila kuchoka, wakiimba nyimbo za chama na kutaja jina la CCM na Dk Samia mara kwa mara.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button