Walanguzi mazao ya wakulima kubanwa

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ametangaza mpango wa serikali kufungua vituo vya ununuaji mahindi mkoani Njombe, ikiwa ni mkakati wa kudhibiti ulanguzi.

Kauli hiyo aliitoa baada ya mgombea ubunge Jimbo la Makambako, Daniel Chongolo kuomba serikali ifungue vituo vya ununuzi mazao katika jimbo hilo hasa kutokana na walanguzi kuwalangua wakulima.

Akihutubia wananchi kwenye mkutano wa kampeni katika Mji wa Makambako mkoani Njombe, Samia alisema ndani ya mwezi huu, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) utafungua vituo vya ununuzi mazao.

“Nataka niwape habari njema kwamba ndani ya mwezi huu pengine kuanzia wiki ijayo, tutafungua vituo vya kununulia mahindi ndani ya Mkoa huu wa Njombe. Sasa vitakuwa maeneo gani itaamuliwa baadaye lakini ndani ya mkoa huu tutafungua vituo,” alisema.

Kuhusu ombi la Chongolo kuwasilisha andiko mradi wa uzalishaji umeme kwa nguvu ya upepo, Samia alisema wasaidizi wake wapo tayari kulipokea na watalifanyia kazi ili kuongeza nguvu katika ajenda ya nishati safi.

“Kwa hiyo tupo tayari kulipokea andiko, tutalipitia na tuone linalowezekana,” alieleza.

Kwa upande wa ujenzi wa kituo cha pamoja cha forodha, alisema suala hilo serikali italifanyia kazi kwani Makambako ni mji mkubwa kibiashara.

“Tumewataka TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kurekebisha mifumo yao, lakini la pili tumeunda tume kutushauri mambo ya kodi, tutakapopokea ripoti yao, Makambako itafikiriwa katika hayo mapendekezo,” alisema.

Aidha, Samia alisema amepokea maombi kuhusu bandari kavu kwa ukanda wa Nyanda za Juu Kusini na kuahidi kulizingatia suala hilo.

“Kwa ukanda huu nimeanza Songwe kuna bandari kavu, Mbeya nimepita wanaomba bandari kavu, Njombe wanaomba bandari kavu, sasa nikifika Iringa labda wataomba bandari kavu. Ninakwenda nalo kuona wapi hasa tuweke bandari kavu lakini lile la Songwe limeshapitishwa,” alisema.

Mgombea huyo pia alikipongeza Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuanza mchakato wa kujenga tawi la chuo hicho katika Mji wa Njombe.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button