Huduma zinazogusa wananchi kuimarishwa

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuimarisha huduma zinazogusa moja kwa moja wananchi na kuwa utekelezaji wa huduma hizo hautakuwa na mjadala.
Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na sekta ya elimu, afya, maji na umeme huku akisisitiza kuwa yeye haongozi wanyonge bali anapeleka miundombini ya kuwainua kiuchumi.
Alisema pia serikali yake haitaacha mtu aharibu zao la chai.
Akizungumza kwenye mikutano ya kampeni eneo la Nyororo wilayani Mufindi, Mafinga na Kalenga mkoani wa Iringa, Samia alisema endapo watapata ridhaa ya wananchi kuunda serikali na kusisitiza kuwa watahakikisha kila Mtanzania anafikiwa na huduma hizo.
“Pia, tutahakikisha kila mtoto wa Kitanzania anakwenda shule na kama mnavyojua elimu yetu tunaitoa bila ada, tutakwenda na mwendo huo huo kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita. Na anapokwenda chuo kikuu mkopo atakuta tayari ili aende chuo kikuu.
“Mkitupa ridhaa yenu ya kuunda serikali na kuongoza nchi niwahakikishie kazi ile ile tuliyokwenda nayo miaka mitano iliyopita ni kasi ile ile tutaenda nayo miaka mitano ijayo… pia tunataka kila Mtanzania afikiwe na huduma ya afya na kwa asiye na uwezo tumesema serikali itakwenda kumsaidia, tunataka kila Mtanzania awe na umeme ili kurahisisha huduma zake nyumbani zikiwemo za kiuchumi, lakini pia kulinda usalama wao, kwani umeme ni usalama wetu,” alisema.
Akiwa katika mikutano hiyo, pia aliahidi kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja ili kurahisisha usafirishaji wa watu, bidhaa na mazao.
Aidha, akiwa Mufundi, Samia alizungumzia suala la madai ya wafanyakazi wa Kiwanda cha Mgololo na alisema pamoja na kuwa siku za nyuma serikali na mwekezaji waliwalipa, serikali imepokea madai mapya ambayo yanakwenda kuhakikiwa na kuahidi kuwa yatakayokuwa halali yatalipwa na hakuna atakayepunjwa.
Alisisitiza pia mwekezaji wa mashamba na kiwanda cha chai cha Mufindi, Kampuni ya DL Group ameanza kulipa madai ya wakulima ya takribani Sh bilioni 2.7 sambamba na stahiki za wafanyakazi na kufufua kiwanda.
Samia alisisitiza kuwa serikali imeunda timu inayofanya tathmini ya kina kuhusu mashamba na viwanda vya chai kote nchini na endapo wawekezaji hao wataonesha kushindwa serikali itayachukua.
Akiwa Mafinga, Samia aliahidi akipata ridhaa ya wananchi wataanzisha kongani za viwanda kwa vijana ikiwemo na viwanda vya misitu na vya kuongeza thamani ya mazao ili kupata soko la ndani na kimataifa.
Alisema pia serikali itakwenda kujenga maghala ya kuhifadhi mazao sambamba na NFRA, itaanza kununua mahindi kwa wakulima baada ya kumaliza kazi hiyo katika mikoa ya Ruvuma na Rukwa.
Pia, aliahidi kujenga stendi ya kisasa ya Mafinga.
Akiwa Jimbo la Kalenga, Samia alisema tangu kuanza mikutano ya kampeni mambo yanayozungumzwa ni yale yanayowagusa wananchi hususani wa vijijini.
“Kuna maneno wanasema hii serikali si ya wananchi, na mimi nimewajibu siongozi wanyonge, mimi naongoza Watanzania, tumejipanga kuwajengea Tanzania tunayoitaka, tumepeleka huduma za kijamii vijijini, ndio kumjali mnyonge,” alisema.