CHAUMMA kuboresha miundombinu ya kilimo

KILIMANJARO; MGOMBEA urais wa Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu amesema iwapo chama hicho kitachaguliwa kuingia madarakani, kipaumbele cha serikali yake kitakuwa ni kuboresha miundombinu katika maeneo ya uzalishaji kupitia kilimo.
Mwalimu alitoa kauli hiyo juzi katika Viwanja vya Manyema wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wakati wa mkutano wa kampeni za chama hicho uliokwenda sambamba na uzinduzi wa kampeni za chama hicho Jimbo la Moshi Mjini.
“Kilimo ni nguzo kuu ya ukuaji wa uchumi lakini miundombinu katika maeneo ambayo shughuli za kilimo zinafanyika sio mizuri,” alisema.
Alisema kukosekana kwa miundombinu katika maeneo ya shughuli za kilimo ndiko kunakosababisha bei ya vyakula kuwa juu.
“Barabara zinazoelekea katika maeneo yenye shughuli za kilimo si nzuri, jambo ambalo linawafanya wasafirishaji kuwatoza wakulima bei kubwa ya kusafirisha mazao ya kilimo na yakifika sokoni wakulima nao huyauza kwa bei ya juu,” alisema.
Aliongeza: “Tunachoshuhudia kwa sasa ni uimarishaji wa miundombinu mijini ili wananchi waende maofisini kwa raha huku tukiwasahau wale (wakulima) ambao wanazalisha chakula kinachowapa nguvu ya kwenda kufanya kazi”.
Aidha, Mwalimu alisema serikali yake pia itajikita katika ujenzi wa mtandao wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Arusha kupitia Wilaya ya Moshi, kwa lengo la kukuza uchumi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambayo alisema ina fursa nyingi za kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya utalii na sekta nyinginezo, ikiwemo kilimo.
Katika mkutano huo wa kampeni, Mwalimu alimtambulisha mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya Chaumma, Patrick Assenga na wanaowania nafasi ya udiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.