Watuhumiwa 940 dawa za kulevya mbaroni

DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata kilo 33,077 za dawa za kulevya aina mbalimbali na kuwashikilia watuhumiwa 940 kuhusiana na matukio tofauti ya biashara haramu ya dawa hizo.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema leo jijini Dar es Salaam kuwa katika msako huo pia walikamata kilo 4,553 za mbegu za bangi, silaha mbili za moto zikiwa na risasi 11, magari tisa, pikipiki 26 na bajaji mbili. Aidha, ekari 64 za mashamba ya bangi zimeteketezwa.

Lyimo alisema miongoni mwa matukio hayo, operesheni iliyofanyika Manzese, mtaa wa Tupendane, ilikamata watu watatu akiwemo raia wa Lebanon wakiwa na kilo 2.4 za Cocaine. Dawa hizo ziliingizwa kutoka Brazil kupitia Kenya na Uganda kwa njia ya kumezwa kabla ya kuingizwa Tanzania.

Katika tukio jingine, maofisa wa DCEA walikamata sigara 50 za kielektroniki zenye bangi katika klabu ya “Bad London” Temeke na “Sanaa Reggae Bar” Masaki. Sigara hizo zilikuwa zikitoka Uingereza na zilihusisha kemikali hatarishi zenye madhara makubwa kiafya ikiwemo saratani na magonjwa ya akili.

Aidha, katika eneo la Bahari Beach jijini Dar es Salaam, raia wa Marekani na mke wake Mtanzania walikamatwa na chupa 11 za dawa aina ya Ketamine pamoja na bangi. Kamishna Lyimo alisisitiza kuwa hatua za kisheria zinaendelea dhidi ya watuhumiwa wote waliokamatwa. SOMA: Tani 18 dawa za kulevya zadakwa Dar

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button