TRA yazindua dawati la uwezeshaji biashara Iringa

IRINGA: Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa imezindua Dawati Maalumu la Uwezeshaji Biashara, hatua inayolenga kuboresha mahusiano kati ya serikali na wafanyabiashara sambamba na kuimarisha utamaduni wa ulipaji kodi kwa hiari.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Peter Jackson, alisema dawati hilo litakuwa chanzo cha elimu ya kodi, ufafanuzi wa sheria, pamoja na msaada wa kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa ngazi zote.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, aliwataka wafanyabiashara kutumia kikamilifu huduma zitakazotolewa, akisisitiza kuwa dawati hilo ni jukwaa muhimu la mawasiliano litakalojenga uelewa wa pamoja kati ya serikali na sekta binafsi.

Akizindua dawati hilo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, aliipongeza TRA kwa hatua hiyo akisema ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuboresha mazingira ya biashara.

Aliwahimiza wafanyabiashara kutoa risiti na wananchi kudai risiti ili kuimarisha mapato ya taifa na kuchochea maendeleo.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) mkoa wa Iringa, Kessy Ndandu, alisema dawati hilo limefungua ukurasa mpya kwa wafanyabiashara wadogo kupata uelewa wa kodi na mbinu za kukuza biashara kwa kuzingatia sheria.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi wa serikali, viongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara (JWT), viongozi wa masoko, taasisi mbalimbali za umma na binafsi pamoja na wananchi wa mkoa wa Iringa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button