Wezi wa pembejeo wanaswa Mtwara

MTWARA: JESHI la Polisi mkoani Mtwara linawashikilia watuhumiwa 13 kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa pembejeo za korosho za ruzuku za  wakulima wa zao hilo zilizogharimu zaidi ya Sh milioni 15.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habar, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara SACP, Issa Sulemani amesema Agosti 29 mwaka huu jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ikiwemo Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) ilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 13 ikiwemo viongozi wa vyama vya msingi vya Halmashauri ya Mji Nanyamba (AMCOS) pamoja na watumishi wa serikali.

Amesema watuhumiwa hao wamekuwa wakijihusisha na wizi wa pembejeo hizo za ruzuku za serikali kwa kutoa kwa wakulima ambao sio wakazi wa maeneo husika (wakulima hewa) na kufanya kuwepo na upotevu wa pembejeo za maji lita 308 na salfa ya unga mifuko 12 aina ya simba ambapo hizo zote zina thamani hiyo ya zaidi Sh milioni 15.

”Wapo baadhi ya watuhumiwa hao wamekuwa wakifanya hivyo kwa misimu tofauti tofauti hivyo natoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara kuacha kujihusisha na wizi wa pembejeo za wakulima wa korosho na mazao mengine,”amesema Sulemani.

Amesema kwasasa uchunguzi unaendelea na utakapo kamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani na kwa kuwa suala hilo ni kosa kisheria jeshi hilo la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama havitasita kuwachukulia hatua watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo vya uhalifu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa CBT, Francis Alfred amesema uwepo wa baadhi ya viongozi hao wa Amcos kufanya udanganyifu huo kunaathiri jitihada za serikali za kumpatia pembejeo mkulima ruzuku ya asilimia 100.

“Nalishukuru jeshi la polisi Mtwara kwa ushirikiano wao na tunaahidi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi katika mikoa mingine kuhakikisha kuwa wote wanaofanya udanganyifu wa pembejeo wanachukuliwa hatua,”amesisitiza Francis

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button