Wakulima Kilimanjaro waonywa ung’oaji miche ya kahawa

KILIMANJARO: MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amepiga marufuku wakulima kung’oa miche ya kahawa, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda zao hilo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wakazi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
Nurdin Babu ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa msimu wa 6 wa Kahawa Festival 2025, unaotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 3 hadi 5 mwaka huu mkoani Kilimanjaro, ukiwa na kauli mbiu “Kahawa ni Ibada.”
Amesema kwa Mkoa wa Kilimanjaro kahawa ni zao mama linaloleta maendeleo ya kiuchumi na kielimi, lakini kuna baadhi ya wananchi huko milimani wang’oa miche ya zao hilo kwa lengo la kujenga nyumba.
“Ni marufuku kukata kahawa, ukikata ya zamani aliyootesha Babu yako panda miche mipya katika maeneo hayo, tusipofanya hivyo hatuwezi kwenda, hata kama mti umeupanda wewe umehangaika nao, ni marufuku kuukata mpaka upewe kibali na mkuu wa wilaya,” amesema.

Akizungumzia Tamasha la Kahawa Festival, Babu amesema lengo ni kuhamasisha jamii kutambua fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa kahawa, kufufua uzalishaji wa zao hilo, na kutoa elimu juu ya faida za kiafya na kiuchumi zinazotokana na kahawa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Primus Kimaro, amesema Kahawa Festival inawakutanisha wadau wa kahawa kuanzia wakulima hadi walaji, kuonyesha ubora wa zao hilo, kuhamasisha unywaji wa kahawa na upatikanaji wa soko la ndani na nje, kuboresha chapa (branding), na kukuza utalii kupitia utamaduni wa utengenezaji na unywaji wa kahawa.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU), Julius Mollel, ameiomba serikali kutunga muswada wa sheria ya kulinda zao la kahawa, ikiwemo kupiga kuweka utaratibu wa mkulima kupata kibali kabla ya kukata mti wa kahawa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Tamasha hilo, Dennis Maulu, amesema kutakuwa na maonesho mbalimbali, mashindano ya utengenezaji na uonjaji wa kahawa pamoja na elimu kuhusu fursa katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.



