UDP yaahidi kusimamia matumizi sahihi rasilimali za nchi

GEITA: CHAMA Cha siasa cha UDP kimeahidi kuwa iwapo kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kitahakikisha kuwa kinasimamia matumizi sahihi ya raslimali za nchi.
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia UDP, Saum Hussein Rashid ametoa ahadi hiyo Septemba 10, 2025 wakati akinadi sera za chama hicho katika viwanja vya soko la Nyankumbu mjini Geita.
Saum amesema Tanzania imebarikiwa raslimali nyingi ikiwemo madini, maji na aridhi yenye rutuba ambayo iwapo zitatumika kwa ufasaha kila mtanzania anayo nafasi ya kuchangia katika maendeleo ya taifa.
Ametolea mfano raslimali madini ambayo ipo kwa uwingi mkoani Geita iwapo itatumiwa kwa ufasaha ni fursa na kichocheo kikubwa kinachoweza kuonhgeza mapato ya ndani na kuboresha huduma za kijamii.

Amesema chama kimejipanga kwa mikakati thabiti, ikiwa lengo kubwa ni kuwainua wananchi watanzania, kwa kuwafungulia fursa za kiuchumi kwa kuweka miundombinu Rafiki ya kilimo, madini na usafirishaji.
“Raslimali hizi za madini zilizopo Geita lazima tuhakikishe zinawanufaisha watanzania wote, na hasa wazawa, hasa kwa kuanza kuwainua wachimbaji wadogowadogo kwa kuwapatia mitaji.
“Kama tunauwekezaji, uwezekuwa ni uwekezaji wenye tija, ambayo wazawa watafaidika, na wawekezaji watafaidika, lazima tutoe ruzuku ambayo itawanufaisha wachimbaji wadogo.
“lakini pia lazima tuwe na vifaa vya kutosha, vya utafutaji wa madini, kuchimba na hatimaye kuchakata ili raslimali hii iweze kuwa na ubora kabla ya kutoka nje ya mipaka ya Tanzania”, amesema Saum.
Ameongeza kuwa pia kupitia raslimali maji ya ziwa viktoria na maziwa mengine nchini UDP itasimamia matumizi bora ya maji ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa watanzania wote.
“Lengo kubwa tunaposema tunamtua mama ndoo kichwani, maana yake tuonyeshe uhalisia, kama tunavyojua Geita ipo karibu na ziwa Viktoria, haiwezekani mpaka sasa kuwe na changamoto ya maji.

“Katika wakati huu tulionao hatutaki kuona kuna changamoto ya maji, kwa sababu maji yapo ziwa Viktoria, tutaanza kwa kuweka miundombinu ya kuvuna maji ya mvua kuhakikisha tunakuwa na maji ya kutosha.
“Tumejipanga kuhakikisha tunachimba visima virefu vya maji, kwenye maeneo yote ili kuondokana na changamoto hii ya maji, kwa kuwa tunafahamu maji kuwa ndio uhai wa maisha yetu,” amesema Saum.
Saum ameeleza kuwa kupitia raslimali aridhi iliyopo UDP itahakikisha inawezesha kilimo bora kwa usambazaji wa pembejeo za kilimo kwa bei Rafiki na kuwafikia wakulima kwa ajili ya kilimo chenye tija.
Amesema pia UDP imejipanga pia kuhakikisha inajenga kiwanda kila mkoa ili kupandisha thamani ya mazao ya chakula na biashara na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa zima kwa ujumla.
“Raslimali za uchumi tunazo, tunataka, wasimamizi wazuri, kwa maana ya madiewani, wabunge na endapo mtatuaamini na kutupa ridhaa tutakwenda kuyatekeleza haya ndani ya muda mfupi”, amesema.



