Takukuru yatoa angalizo wasimamizi wa uchaguzi Geita

GEITA: TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita imewataka wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata na majimbo kulinda thamani ya kura kwa kuepuka udanganyifu wa aina yeyote.

Aidha, wasimamizi hao wa uchaguzi wametakiwa kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa ili kuepuka vitendo vya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, James Ruge ametoa maagizo hayo Septemba 11, 2025 katika semina maalum kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi iliyofanyika katika ofisi za Takukuru mkoani humo.

Ruge amesema rushwa ina madhara makubwa katika uchaguzi ikiwemo kugeuka kikwazo na kuwakosesha wananchi haki ya kupata viongozi bora na wenye dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo.

Ruge amesisitiza kuwa jukumu la wasimamizi hao ni kuhakikisha haki inatendeka kwa wagombea wote, kuzingatia maadili ya uchaguzi na kuepuka kushiriki au kufumbia macho vitendo vyote vya rushwa.

Ameonya kuwa Takukuru haitosita kuhukua hatua kali dhidi ya yule atakayehusika kwenda kinyume na kisheria kwa kuwa vitendo vya rushwa havina nafasi katika mchakato wa uchaguzi huru na wa haki.

“Uchaguzi ni fursa ambayo watu wanaitumia kutafakari mustakabari wa maisha yao, kupitia fursa hii inawawezesha wananchi kujua, wamchague mgombea yupi kati ya wagombea walijitokeza”, amesema.

Ofisa wa Takukuru mkoa wa Geita, Said Lupunjaje amesema ni jukumu la msimamizi wa uchaguzi kama ilivyo kwa raia mwingine wa Tanzania kubeba suala la uchaguzi kwa uzalendo kwa maslahi ya umma.

Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya wilaya ya Geita, Sarah Yohana alisema wamejidhatiti kusimamia sheria za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na miongozo ya Takukuru kulinda haki ya mpiga kura.

Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata, Mpanduji Charles, alisema maelekezo ya Takukuru ni sehemu ya kuwakumbusha juu ya tahamni ya kura katika uchaguzi mkuu na hivo hayapaswi kupuuzwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button