Zijue ngoma za Wangindo
WANGINDO ni miongoni mwa makabila yanayopatikana katika Mkoa wa Lindi ambao upo Kusini mwa Tanzania.
Mbali na Wangindo, mkoa huo una mchanganyiko wa makabila mbalimbali ambayo miongoni mwao, mila na tamaduni zao hushabihiana.
Kwa mujibu wa Tovuti ya Mkoa wa Lindi, makabila mengine katika mkoa huo ni pamoja na Wamakonde, Wamatumbi, Wamachinga, Wamakua na watu wachache wenye asili ya Asia na Kiarabu.
Makala haya leo yanazungumzia Kabila la Wangindo ambalo pia hupatikana katika mikoa ya Morogoro na Pwani. Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, awali watu wa Kabila la Wangindo walikuwa katika Mkoa wa Lindi, huku utamaduni wao ukishabihiana kwa karibu zaidi na ule wa Wamatumbi.
SOMA: “Jamii zidumishe tamaduni kuvutia watalii”
Wangindo hujishughulisha zaidi na kilimo cha mahindi, mtama, uwele na viazi vitamu. Awali, walikuwa wakijishughulisha na uwindaji, wakipatikana zaidi zaidi katika mapango waliyoyaita ‘mbako’. Kwa sasa Wangindo na Wamatumbi wengi wanapatikana maeneo ya Rufiji, Mkuranga, Madaba, Ndapapata, Kibata, Mbemkulu, Ngarambe, Ilonga, Kibaha na Liwale.
Uchunguzi wa gazeti la HabariLEO umebaini kuwa, kama ilivyo kwa watu wa makabila mengine, Wangindo pia wana utamaduni wao wa asili unaoonekana katika mambo mbalimbali kama vile chakula, mavazi, ngoma za asili, mila pamoja na desturi.
Miongoni mwa mambo ya utamaduni wa watu wa kabila hili ni ngoma za asili zinazochezwa katika matukio tofauti, hasa wakati wa furaha kama harusi, sikukuu, jando na unyago, matambiko, matibabu ya asili na wakati wa mavuno.
Ingawa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia hususani masuala ya utandawazi, mila na desturi za makabila mengi zinapotea. Utamaduni wa Wangindo, hususani suala la ngoma umeendelea kusalia na wenyewe wanaendelea kuuendeleza.
Katika mazungumzo na HabariLEO, mmoja wa watu wa kabila hilo kutoka Kijiji cha Bigwa, Kata ya Mwarusembe wilayani Mkuranga (Mkoa wa Pwani), Rashid Salum anataja baadhi ya ngoma za kabila lao kuwa ni ngoma ya Mandilu, Manyanga, Ngende Liwale, Lizombe na Gombe Sugu ambayo ndiyo ngoma pendwa ya Kabila la Wangindo.
Makala haya yanagusia baadhi ya ngoma za kabila hilo miongoni mwa nyingi ikianza na Ngoma ya Mandilu.
Mandilu
Salum anasema ngoma hii huchezwa wakati wa matibabu ya asili kutoka kwa mganga wa jadi, hasa mtu anapopata changamoto za maradhi. “Kwa kawaida ngoma hii huchezwa wakati wa shida, yaani mtu anapokuwa mgonjwa. Akienda kutibiwa, basi inapigwa huku matibabu yakiendelea…”
Anasema hata jamii inapopita katika shida mbalimbali, wanapotaka kufanya ibada za matambiko ngoma hii ndiyo hutumika sana pamoja na ile ya Manyanga.
Madogoli
Kwa mujibu wa Salum, Wangindo wana ngoma nyingine inayojulikana kwa jina la ‘Madogoli.’ Anasema hiyo ni ngoma inayotokana na mwingiliano na Kabila la Wamatumbi. Ngoma hiyo huchezwa kwa ajili ya kumtibu mtu mwenye mapepo, jamii inapofanya matambiko ya kimila.
Ngende Liwale
Ngoma hii huchezwa wakati wa mavuno au wakati wa kuomba dua mbalimbali za watu wa Kabila la Wangindo zinazofanyika katika maeneo ya milimani. Wakati wa kucheza, wachezaji hutumia mkia wa nyumbu.
“Sisi tunatumia mkia wa nyumbu kuomba kwenye Ngende Liwale kule kwenye Mlima Nanyumbu,” anasema. Anaongeza: “Sasa tupo kwenye vizazi vya kisasa, kuna watu hawajui mila na desturi. Tunatumia mkia huu, mkia halisi wa nyumbu tuliokabidhiwa kutengenezea utamaduni kwa ajili ya vizazi vyetu ili vijue kuna ngoma yao ya Ngende Liwale.”
Gombe Sugu
Ngoma nyingine pendwa ni Gombe Sugu. Kwa Wangindo, ngoma hii huchezwa wakati wa furaha, kwenye sherehe za mavuno, jando na sherehe za unyago na huchezwa na watu wa jinsia zote.
Kwa mujibu wa Salum, katika sherehe za mavuno au sikukuu, ngoma hiyo inapochezwa mara nyingi huambatana na vyakula mbalimbali vya asili na pombe za kienyeji ambazo pia hazikosekani. “Mara nyingi huwa tunakuwa na vyakula vya kiasili, hasa vile vya kitamaduni na pombe ya mtama ndiyo hutumika zaidi,” anasema.
Salum anasema ngoma nyingi huchezwa wakati wa sherehe, hasa kipindi cha mavuno kinachotokea Agosti hadi Oktoba.



