Aspa kuimarisha ustawi wa afya ya punda Geita

GEITA: SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Arusha Society for the Protection of Animals (ASPA) limeanza utekelezaji wa mpango maalum unaolenga kuimarisha ustawi wa afya ya wanyama kazi aina ya punda mkoani Geita.
ASPA inatekeleza mpango huo chini ya ufadhili wa Shirika la Brooke East Africa dhamira ikiwa ni kuhakikisha mazingira salama ya kiafya kwa punda ambao ni miongoni mwa wanyama waliosahaulika.
Mkurugenzi wa ASPA, Livingstone Masija amewasilisha mpango huo mbele ya waandishi wa habari baada ya kutembelea eneo la wachimbaji wadogo Mgusu ambapo punda hutumiwa zaidi kubeba mizigo.
Amesema mpango unatekelezwa kupitia uwezeshaji wa elimu ya mazingira salama na huduma stahiki ya afya ya wanyama inayotolewa na maofisa mifugo, madaktari wa wanyama na maofisa wa ASPA.

Amesema elimu kubwa inayosisitizwa ni vipimo vya joto la wanyama ikiwemo punda ili kubaini dalili za ugonjwa na kuachana na tabia ya utoaji holela wa dawa za mifugo pasipo kujua changamoto za kiafya.
Amesema vipimo sahihi vya joto la wanyama wa kufuga ndio njia sahihi ya kubaini iwapo mnyama anakabiliwa na magonjwa ama ni mabadiliko ya hali ya hewa hivo kuepuka dawa zenye athari kubwa.
“Ukishajua joto la mwili unatafuta dawa za kutuliza maumivu, na dawa za kushusha joto baadaye ndio unaweza kuanza kujua ushughulike na tatizo la mnyama huyo kwenye eneo gani”, amesema Livingstone.
Amesema pia matibabu ya Wanyama ikiwemo punda yanapaswa kutolewa kwa ushauri wa watalaamu kwa kuzingatia aina ya mnyama badala ya kutoa dawa kwa mazoea jambo ambalo ni hatari.

Daktari wa Wanyama wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Dk Jasson Mutayabarwa amesema wanashirikiana na ASPA kufanikisha mpango huo kwa kuwashirikisha maofisa mifugo wa kata zote.
Mjumbe wa Bodi ya Chama Cha Ushirika Mgusu, Eric Joseph amekiri kuwa ASPA imesaidia usatwi wa punda ambao wanafanya kazi ya kubeba mizigo mgodini hapo toafuati ilivyokuwa hapo awali.
Amesema utaratibu uliowekwa ni kuwa kila gharama ya punda mmoja kubeba mzigo wa mawe mgodini kwa safari moja ni sh 1,000 ambayo hulipwa kwa majumuisho ya kazi ya jumla kwa mmiliki kwa punda.
Mfugaji wa Punda katika eneo la Mgusu, Simon Bukombe amekiri kuwa mbali na elimu ya afya pia elimu ya kuzingatia masaa ya kazi kwa punda imesaidia punda wake kusalia na afya njema kwa kazi za kila siku.



