Jasmine Ng’umbi aahidi kusukuma maendeleo ya vijana

IRINGA: Mbunge Mteule wa Viti Maalum Vijana Taifa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka mkoa wa Iringa, Jasmine Ng’umbi, ameahidi kutumia nafasi yake bungeni kama kichocheo cha sera na miradi inayoongeza fursa za maendeleo kwa vijana na wanawake nchini.
Akizungumza leo katika uzinduzi wa kampeni za wagombea ubunge na udiwani katika majimbo ya Kalenga na Iringa Mjini, uliofanywa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira, Jasmine alisema dhamira yake kuu ni kuhakikisha makundi hayo yanapata nafasi kubwa zaidi kiuchumi na kijamii.

“Nitashirikiana na Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na wabunge wenzangu kuhakikisha tunatunga na kusimamia sera zenye matokeo chanya kwa vijana na wanawake—kuanzia upatikanaji wa mitaji midogo, ujuzi wa kisasa, hadi ushiriki wao katika miradi mikubwa ya maendeleo,” alisema Jasmine.
Aliwaomba wananchi wa Iringa na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuiamini CCM kwa kumpa kura za kishindo Rais Samia, wagombea ubunge na madiwani, akisema chama hicho kimeonyesha kwa vitendo kuwa ni chachu ya maendeleo kwa wote bila ubaguzi.
“Rais Samia ameonesha mfano wa uongozi wa vitendo. Ni jukumu letu kuendeleza kasi hiyo kwa kuhakikisha CCM inaendelea kupewa ridhaa ya kuongoza, ili vijana, wanawake na Taifa kwa ujumla waendelee kunufaika,” alisisitiza Jasmine.



