Watoto wa Ilomo wamuomba RC Iringa kuingilia mgogoro wa mirathi

Sarah Agustino Ilomo, mmoja wa watoto wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa Iringa, marehemu Mzee Augustino Ilomo, amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, kuingilia kati mgogoro wa mirathi unaotishia kupoteza mali zote zilizoachwa na baba yao.

Sarah anadai kuwa, licha ya juhudi mbalimbali zikiwemo za kisheria, mchakato wa kugawa urithi umegeuka chanzo cha maumivu baada ya baadhi ya mali kuuuzwa kwa njia anazodai kuwa za udanganyifu, bila ridhaa ya watoto wote wa marehemu.

Amesema Mzee Ilomo, aliyefariki dunia mwaka 2016, alikuwa mfanyabiashara mkubwa wa usafirishaji wa abiria na huduma za hoteli kupitia kampuni yake ya Living Light.

Aliacha watoto 12 na mali zikiwemo nyumba saba—moja jijini Dar es Salaam na sita mjini Iringa—viwanja viwili (Igumbilo na Kilolo), magari matatu (Land Rover Discovery, Toyota Pickup na Canter) na zaidi ya Sh milioni 160 benki.

Awali, amesema familia ilimteua mdogo wa marehemu, Michael Ilomo, kuwa msimamizi wa mirathi, hata hivyo, miezi sita baadaye mama wa kambo (jina limehifadhiwa) alitengua uteuzi huo bila maridhiano.

Kwa mujibu wa Sarah, kabla taratibu za mirathi hazijakamilika, baadhi ya watoto wakiungana na mama wa kambo wameshauza nyumba tano, magari yote matatu na viwanja viwili bila kushirikisha wengine.

Kinachotia hofu zaidi, anasema, kuna mpango wa kuuza nyumba mbili pekee zilizobaki, ikiwemo jengo la ghorofa nne lililokuwa hoteli ya Living Light na kwa sasa linatumika kama hosteli za wanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Ruaha, pamoja na nyumba nyingine iliyo katika mtaa wa kibiashara wa Uhindini mjini Iringa.

Sarah anadai nyumba hizo zinataka kuuzwa ili kulipa deni la zaidi ya Sh milioni 460, linalotokana na mkopo wa Sh milioni 250 uliodaiwa kuchukuliwa na mama wa kambo kwa sababu zisizojulikana, deni ambalo limeongezeka maradufu.

“Nyumba tano zimekwishauzwa na sasa wanachotaka ni kuuza hizi mbili zilizobaki ili kulipa deni hilo. Tutakimbilia wapi watoto wa marehemu kama nyumba hizo pia zikiuzwa?” alihoji Sarah kwa uchungu.

Anadai mauzo hayo yamefanyika kwa kutumia nyaraka za kughushi, zikiwemo za wosia, kampuni na hati za umiliki.

Anaeleza kuwa wosia wa baba yao, ambao awali ilidaiwa umehifadhiwa kanisani, haukuwasilishwa kwa familia kwa muda mrefu, na baadaye wakabaini nyaraka zimeghushiwa ili kuonyesha ni watoto wachache pekee wananufaika.

Sarah pia ameeleza kuwa fedha zilizokuwa benki zimepotea bila maelezo, na juhudi za kufuatilia hazijafanikiwa.

“Tunazo taarifa za wazi za nyaraka feki na mauzo kabla mirathi haijakamilika, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa. Mali za marehemu zinaendelea kuuzwa pamoja na kulifanyia kazi suala hilo kwenye mamlaka mbalimbali,” amedai.

Kwa niaba ya baadhi ya watoto wa Mzee Ilomo, Sarah amemuomba Rais Dk Samia Suluhu Hassan, kupitia Mkuu wa Mkoa wa Iringa, kuingilia kati ili kulinda haki za watoto wa marehemu.

Lakini pia amewaomba wadau wengine watetezi wa haki za binadamu kikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kuwasaidia kupata haki zao zinazoendelea kupotea.

“Tunaomba msaada wa haraka, vinginevyo tutapoteza kila kitu tulichoachiwa na baba yetu,” amesisitiza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button