Wabunifu majengo wafundwa tahadhari kwa jamii

DAR ES SALAAM: WABUNIFU Majengo na Wakadiriaji Majenzi wametakiwa kuhakikisha kila mradi wa maendeleo wanaousimamia unazingatia ubora na usalama ilikuepuka hasara na kuliinda jamii dhidi ya majanga yatokanayo na majengo.

Wito huo umetolewa mkoani Dar es salaam na Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi na Umeme kutoka Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Mwanahamisi Kitogo wakati akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi, Balozi Aisha Amour kwenye mahafali ya pili ya wataalamu waliokidhi vigezo kuanzia Oktoba 2024 hadi Mei 2025.

“Kwa sasa ninyi ni wataalamu mliokidhi vigezo na mmetambuliwa rasmi na bodi ya usajili. Heshima hii si yenu peke yenu, bali ni sehemu ya mchango wenu katika maendeleo ya taifa letu kupitia sekta ya ujenzi,” amesema Mhandisi Mwanahamisi.

Amebainisha kuwa wabunifu majengo na wakadiriaji majengo ni nguzo muhimu katika kuhakikisha miradi inakidhi ubora, kwasababu sanifu, hesabu na makadirio ya gharama wanayofanya yanahusiana moja kwa moja na usalama wa maisha na mali za jamii inayowazunguka.

“Msichukue mradi wowote bila kufuata kanuni na maadili ya kitaaluma pamoja na sheria na miongozo ya nchi. Kila mradi unaosimamiwa kwa weledi unaokoa maisha na mali,” amesisitiza.

Mwanahamisi amewahimiza wahitimu kufanya kazi kwa uadilifu, uwazi na heshima, huku wakiepuka kutumia nafasi zao kwa masilahi binafsi. Aidha, aliwataka kuwa mfano wa kuigwa kwa vizazi vijavyo kupitia usimamizi wa miradi yenye viwango pamoja na kuendana na mapinduzi ya teknolojia yaliyopo kwa sasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usajili na Maendeleo ya Taaluma, Mhandisi Bundala Robert amesema kuwa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majengo (AQRB) imesajili wataalamu 1,708 na kampuni 489 za kitaalamu kati ya Oktoba 2024 na Agosti 2025.

“Kwa sasa jumla ya wahitimu 170 wamesajiliwa. Kati yao, 35 ni Wabunifu Majengo, 98 Wakadiriaji Majengo, 22 Wasanifu Teknolojia ya Majengo, watatu Wabunifu wa Ndani ya Majengo na wawili Watathmini Majengo na ndio hawa wanaohitimu leo,” amesema Mhandisi Bundala.

Ameongeza kuwa kila mtaalamu ana wajibu wa kusimamia taaluma yake kwa kuzingatia sheria na kanuni, pamoja na kuwa mabalozi wazuri kwa kuhakikisha makadirio na masanifu yanaendana na gharama halisi zinazohitajika.

Kwa upande wake, Mhandisi Patricia Bandora, mhitimu wa fani ya ubunifu majengo, ameishukuru bodi na wadau wa sekta ya ujenzi kwa mchango wao, huku akiahidi kufanya kazi kwa kufuata maadili ya taaluma na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa usalama, gharama stahiki na ubora unaokidhi viwango vya kitaifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button