Wakazi Kasulu kuagana maji yenye matope

KIGOMA: Kukamilika kwa ujenzi wa chujio la maji kutoka chanzo cha Mto Chai na Msemo unaohudumia wakazi wa mji wa Kasulu kunaelezwa kuwa kutaondoa adha ya muda mrefu kwa wakazi zaidi ya 50,000 mji huo kunywa maji yenye tope.
Mkuu wa Wilaya Kasulu,Isack Mwakisu akizungumza mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa,Ismail Alli Ussi wakati mwenge ukizundua chujio hilo alisema kuwa siyo tu kunywa maji yenye tope lakini kutokuwepo kwa chujio kuliwafanya kushindwa kuvaa nguo nyeupe kutokana na hali ya maji ya kufulia kuwa na tope jekundu.

Mwakisu alisema kuwa anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Mamlaka ya maji ya Mji wa Kasulu kukamilisha mradi huo ambao utawafanya kunywa maji safi na salama na meupe ambayo hayana shida kama ilivyokuwa hapo awali.
Kwa upande wake Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mji wa Kasulu (KUWASA), Hussein Nyemba aakitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za mwenge alisema kuwa kiasi cha Sh milioni 385.5 kimetumika kukamilisha mradi huo ambao ulikuwa hitaji kubwa la wakazi 52,527 wa Mji wa Kasulu.

Nyemba alisema kuwa wakati wa mvua nyingi (Masika) hali ndiyo huwa mbaya Zaidi kwa udongo kuporomoka na kuingia kwenye mito hivyo maji kuchafuka Zaidi na kwamba kwa sasa baada ya mradi huo wananchi hao wataondokana na adhabu hiyo.
Akizindua mradi huo Kiongozi wa mwenge wa uhuru mwaka huu, Ismail Alli Ussi alisema kuwa utekekelezaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi unaongeza Imani ya wananchi hao kwa viongozi kwao kuona wanajali changamoto zinazowakabili.

Ussi alisema kuwa serikali kwa kadri inavyoweza imekuwa ikitekeleza miradi hiyo ambayo imepitiwa na mwenge sehemu mbalimbali nchini na kwamba wananchi wanapaswa kuiamini serikali yao kwamba inawajali na kujali shida zinazowakabili hivyo kutatuliwa kwa kadri serikali inapokuwa na uwezo wa kufanya hivyo.



