Wananchi waalikwa tamasha la Nyangumi

MTWARA: WANANCHI mkoani Mtwara na wanaotoka nje ya mkoa huo wameombwa kutembelea kijiji cha Msimbati kwenye Halmashauri ya Wilya ya Mtwara ili kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo kwenye maeneo hayo ikiwemo Nyangumi anaopatikana kwenye hifadhi za bahari.
Hayo yamejiri wakati wa uzinduzi wa Nyangumi Vestival mwaka 2025 msimu wa nne uliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya amesema mkoa huo umebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya kiutalii ambavyo bado havijulikani katika soko la utalii wa ndani na nje ya mkoa na nchi kwa ujumla.
Amevijata baadhi ya vivutio hivyo ikiwemo baadhi ya misitu ya asili aina ya mikoko, hifadhi tengefu za wanyama pori za Lukwika Lumesule na msanjesi katika Wilaya ya Masasi na Nanyumbu, mji mkongwe wa mikindani, fukwe mzuri za Msimbati, Msangamkuu, kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara na vingine.
Aidha, matamasha kama hayo yana umuhimu mkubwa katika kuhakikisha vivutio vilivyopo mkoani humo vinatangazwa na kuwavutia watalii na wawekezaji katika sekta hiyo kutoka ndani na nje ya nchi hivyo wananchi hao wanakaribishwa kutembelea maeneo hayo ili kujionea nyangumi ambao wapo kuanzia Agosti mpaka Novemba kila mwaka.
Kaimu Muhifadhi Mfawidhi wa Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma Amos Singo amesema tukio hilo linaendelea kubadilisha mwonekano wa mkoa huo kwa kuwa mkoa pekee wenye utalii endelevu.
Pia ni miongoni mwa maeneo machache Barani Afrika yenye bahari safi na mazingira ya kuvutia yanayoweza kuwawezesha nyangumi kufika kwa makundi makubwa kila mwaka hasa maeneo ya hifadhi hiyo.
Kwa upande wake Balozi wa Utalii Mkoa wa Mtwara Sameer Murji amesema Nyangumi Festivali siyo tu burudani bali ni jukwaa la kipekee la kuelimisha jamii na kuhamasisha utunzaji wa mazingira ya habari na kuvutia utalii wa ndani na nje ya mkoa huo pia ni hatua kubwa kuelekea ndoto yao ya kuifanya mtwara kuwa lango la utalii wa kusini mwa Tanzania.
‘’Tunaishukuru serikali kwa kutuletea tamasha la nyangumi kila mwaka ila niiombe serikali elimu itolewe zaidi kwa wananchi kuhusu nyangumi baadhi yetu hatumfahamu”ameseme Mariamu Saidi mmoja wa washiriki wa uzinduzi huo