Samia: CCM tutakuza kipato binafsi

ZANZIBAR : MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema wakipewa ridhaa, Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaweka mazin[1]gira yatakayokuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja.

Akizungumza na maelfu ya wananchi waliofurika katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Hamburu, Jimbo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja , Samia amesema moja ya  ahadi ya CCM ni kuendelea kukuza uchumi na kipato cha mwananchi mmoja mmoja, hatua ambayo itawezesha nchi kujitegemea.

“Katika kujenga taifa linalojitegemea, hatutafika huko mpaka kila mtu ndani ya Tanzania yetu, kila kijana awe na shughuli inayompa kipato, yeye mwenyewe asimame kama mtu mmoja,ajitegemee. Aidha, Samia alisema matokeo ya ukuaji uchumi na utekelezaji ahadi za CCM kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, umeonekana dhahiri uwezo wa Dk Mwinyi katika kuwaongoza Wazanzibari.

Alisema maendeleo makubwa yameshuhudiwa Zanzibar. “Pamoja na majanga yote tuliyopitia ikiwemo Covid 19, tumeweza kufanya kazi kubwa pamoja katika sera za kifedha na uchumi na ndiyo maana hatukuweza kukwamisha miradi yetu.”

“Kwenye sera za kifedha na sera za kiuchumi, Dk Hussein (Mwinyi) ameweza kusimamia na kuimarisha uchumi ambao kwa sasa unakuwa kwa kasi kubwa,”alisisitiza. Samia alisema ukuaji uchumi kwa Tanzania bara umeongezeka kwa asilimia sita huku Zanzibar ukiwa juu zaidi kwa asilimia 7.1 kwa mwaka.

“Zaidi uchumi umekuwa hata mifukoni kwa kila mwananchi. Wakati nilipokuwa nikiwasili Nungwi nilikuwa nikitazama kila pande na kujionea namna ambavyo kumejengeka nyumba nzuri za makazi, biashara zinafanyika na mambo yanaenda vyema kwa amani na utulivu,” alisema.

Akizungumzia ukuaji wa sekta ya utalii, Samia alisema idadi ya watalii imeongezeka ambapo watalii zaidi ya milioni tano wamefika Tanzania bara huku zaidi ya watalii 700,000 wamefika Zanzibar ikiwa ni zaidi ya lengo, hivyo aliahidi na kuendelea kukuza sekta hiyo.

Kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Samia alisema kwa kushirikiana na Dk Mwinyi wameweza kunyanyua maendeleo ya watu kutoka kaya maskini kupitia TASAF na kuahidi kuja na awamu nyingine ya mpango huo ili kuendelea kuinua maisha ya Watanzania. SOMA: Dk Nchimbi: Mchagueni Samia aendeleze maajabu

Pia, aliahidi kuendelea na utekelezaji wa miradi kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Samia alisema eneo lingine la kipaumbele ni uchumi wa buluu hususani uvuvi katika bahari kuu na suala la mafuta na gesi. “Suala la mafuta na gesi liko ndani ya uchumi wa buluu tunaendelea kulifanyia kazi kuhakikisha tunakwenda kufaidika na rasilimali hizo,” alisema.

Pia, usafiri na usafirishaji wa watu na mizigo kwa ku[1]tumia Bahari ya Hindi. Alisema mikopo isiyo na riba itaendelea kunyanyua na kuwezesha biashara ndogo zikue na kurasimisha biashara ndogo ndogo Tanzania Bara na Zanzibar. Alisema pande mbili za muungano zimeshirikiana kukuza uhusiano wa kidiplomasia na kukuza jina la Tanzania ulimwenguni. “Heshima tunayoipata ulimwenguni ni kwa sababu ya umoja na mshikamano wetu kama Tanzania na kukuza jina letu,” alisema.

Alisema kwenye masula ya ulinzi na usalama, nchi iko vizuri na kuwahimiza Watanzania kuendelea kudumisha Muungano ambao kwa sasa una miaka 61. Katika hatua nyingine, Samia alisema CCM haina mashaka katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu kwa sababu mambo mengi yamefanyika. “CCM tuna ujasiri kuja kwenu kuomba kura na ujasiri huu unatokana na kwamba tumeweza kufanya mambo makubwa na tunajiamini tutaweza kufanya mambo makubwa,” alisema.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button