Wagombea zingatieni ilani, toeni ahadi zinazotekelezeka

OKTOBA 29, mwaka huu Watanzania watatekeleza jambo kubwa la kidemokrasia na kihistoria la kuwachagua viongozi wa kuwaongoza kwa miaka mitano ijayo kwa kupiga kura.
Utekelezaji huo wa kidemokrasia unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024.
Hili ni tukio kubwa lililobeba hatima ya maisha ya Watanzania, ndiyo maana kwa miezi miwili wagombea watafanya kampeni kunadi sera kupitia ilani za vyama vyao ili kuomba ridhaa ya kuongoza nchi.
Kampeni zilianza Agosti 28 na zitafikia tamati siku moja kabla ya uchaguzi kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar kampeni zitahitimishwa Oktoba 27 kupisha upigaji kura wa mapema kabla ya wa jumla Oktoba 29.
SOMA: Vyama, wagombea wapewa masharti kampeni Uchaguzi Mkuu
Muda wa miezi miwili uliowekwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kufanya kampeni ni wenye umuhimu mkubwa na unatosha kwa wagombea kutoa sera na wananchi kusikiliza, kuchekecha na kupima mgombea yupi anafaa na chama kipi kina uwezo wa kuwaletea maendeleo.
Pamoja na kampeni kufikia mwezi, tunashuhudia baadhi ya wagombea wanafanya kampeni za kejeli, mahoka, vituko na vichekesho wakisahau kwamba Watanzania wa nyakati hizi wanajua kuchuja pumba na mchele kwelikweli.
Tunawakumbusha wagombea urais wa vyama 17 wanaonadi sera katika mikutano ya kampeni, wanaowania ubunge na udiwani kwamba, huu si wakati wa bla bla bali ni nafasi muhimu ya kueleza kile watakachowafanyia Watanzania ikiwa watapewa ridhaa ya kuongoza nchi kwa nafasi husika.
Vipo vyama vinafanya vizuri kwenye kampeni mpaka sasa, tunasikia sera na hoja zinazotekelezeka lakini vipo vingine vinafanya mahoka, hivi havichelewi kuja kupinga matokeo yatakapotangazwa na INEC wakidai wameibiwa kura kumbe walileta mzaha wakasahau Watanzania hawaendekezi mizaha kwenye mambo muhimu yanayobeba mustakabali wa maisha yao.
Kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, wananchi wanahitaji kusikia namna ya utatuzi wa changamoto na utekelezaji wa miradi itakayoinua uchumi wao kama ujenzi wa barabara, reli, kilimo, umeme, shule, maji, afya na utunzaji mazingira.
Watanzania wanahitaji kufahamu namna gani watajikwamua kwenye umasikini kwa kupata mikopo yenye riba nafuu na kuondokana na mikopo umiza na si ahadi hewa ambazo kwa mtazamo wa kawaida, hazitekelezeki.
Tunawakumbusha wagombea kwamba bado siku 39 Watanzania 37,655,559 waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpigakura mwaka huu 2025, wapige kura katika vituo 99,911 kumchagua rais wan chi yetu, wabunge wa majimbo 272 na madiwani katika kata 3,960.