Ushiriki wa wanawake siasa waimarika

MJUMBE Maalum wa Umoja wa Afrika wa Wanawake, Amani na Usalama, Balozi Liberata Mulamula, amesema mwamko wa wanawake kushiriki kwenye siasa na uchaguzi nchini Tanzania unazidi kuimarika na kuonesha matumaini makubwa ya mabadiliko ya kijamii na kisiasa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Balozi Mulamula amesema  tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, idadi ya wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali imeendelea kuongezeka, huku safari hii ikionesha uthubutu wa kipekee. “Mwamko huu si idadi pekee, bali ni ujasiri wa wanawake waliamua kujitokeza, jambo linaloibua matumaini makubwa kwa taifa,” alisema Balozi Mulamula. SOMA: Miaka 30 ya Beijing: Wanawake wanazuiwa mifumo dume

Alibainisha kuwa wanawake wengi wameonesha uwezo wa kujitokeza majukwaani na kunadi hoja zao, huku kura za maoni zikionesha mwitikio chanya kwao, ingawa changamoto zimekuwa zikijitokeza kwenye hatua ya uteuzi.

Mulamula alisema baadhi ya wanawake walioshinda kura nyingi walishindwa kuteuliwa, lakini akaongeza kuwa mazingira yanaanza kubadilika na uchaguzi huu unaweza kuwa wa kipekee ikilinganishwa na miaka iliyopita, kwani mifumo kandamizi ipo mbioni kuondoka.

Aidha, alisema taswira ya nafasi ya mwanamke katika siasa imeiweka Tanzania kwenye hadhi ya juu kimataifa na kusisitiza vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuimarisha hali hiyo kwa kuelimisha jamii kuhusu sheria zinazolinda wanawake.

Changamoto nyingine aliyoitaja ni gharama za kifedha, akisema kampeni zinahitaji mtaji mkubwa ambao umekuwa kikwazo kwa wengi. Alipongeza Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi na kushauri kuundwa kwa mfuko maalum wa kugharamia michakato ya kisiasa ya wanawake.

“Njia ya kudumu ya kujenga kizazi bora ni kupitia elimu ya kujiamini na uzalendo. Kumuelimisha mwanamke ni kuielimisha jamii nzima,” alisema, akisisitiza umuhimu wa elimu bora kuanzia utotoni ili kuandaa viongozi wa baadaye.

Aidha, alishauri mifumo ya upendeleo wa kisheria (quota) iongezwe zaidi ili kuhakikisha ushiriki wa wanawake unapanuka na akahimiza ari na uthubutu wa wanawake uendelee hata baada ya uchaguzi ili kuleta mabadiliko ya kweli ya kimaendeleo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button