HIFADHI YA MACHAPISHO KITAIFA: Nguzo ya urithi wa kitamaduni na kiakili

KATIKA enzi ya mabadiliko ya kidijitali na kasi ya upotevu wa maarifa ya jadi, hifadhi ya machapisho kitaifa imeibuka kama nguzo muhimu ya kulinda urithi wa kitamaduni na kiakili wa Taifa.

Umuhimu wa hifadhi ya machapisho ni kuhifadhi historia ya Taifa kwani yanabeba kumbukumbu za historia, mila, desturi na falsafa za jamii ambazo huunda utambulisho wa taifa.

Machapisho huweka kumbukumbu za simulizi, methali, nyimbo za jadi na imani za jamii ambazo haziwezi kuonekana kwa macho lakini zina thamani kubwa kwa utamaduni. Maktaba za kitaifa zinatoa uwezeshaji wa elimu ya kitamaduni na mtandao jumuishi kwa wanafunzi, watafiti na wananchi wa rika mbalimbali ambao hupata fursa ya kujifunza kuhusu tamaduni zao kwa kina.

Ni ushirikishwaji wa jamii kupitia hifadhi ya machapisho yanayohusisha waandishi, wachapishaji na wasomaji ambao ni mchakato wa kutunza na kuendeleza urithi wa Taifa. Katika kukuza maarifa ya ndani, vitabu na machapisho ya ndani huakisi mazingira ya kitanzania, lugha na changamoto za jamii, hivyo kuchangia maarifa yanayohusiana moja kwa moja na maisha ya wananchi.

SOMA: Chuo Kikuu Huria kuanzisha Shahada ya Utamaduni

Kwa kutambua umuhimu huo katika mkutano wa dunia wa mawaziri wa elimu waliokutana Tehran nchini Iran, moja ya mapendekezo yalikuwa ni kuanzishwa kwa siku ya usomaji duniani ili kuendeleza dhana ya usomaji endelevu. Maadhimisho hayo yaliasisiwa mwaka 1967 katika mkutano wa dunia wa mawaziri wa elimu waliokutana Tehran, Iran chini ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).

Mkutano wa dunia wa mawaziri wa elimu ulipendekeza Septemba 8 kila mwaka iwe ni Siku ya Kimataifa ya Umahiri, inayolenga kufuta ujinga na kuendeleza dhana ya usomaji endelevu. Kwa msingi huo, serikali kupitia Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), imejidhatiti kuhifadhi machapisho yote yanayochapishwa nchini kwa mujibu wa Sheria ya Amana ya mwaka 1975.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya TLSB, Dk Mboni Ruzegea anasema siku ya kimataifa ya umahiri huadhimishwa Septemba 8 kila mwaka, ikiwa ni jukwaa la kimataifa la kutambua juhudi za kukuza umahiri wa kusoma na kuandika duniani.

Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Usomaji Duniani kwa mwaka huu yamefanyika mkoani Morogoro kuanzia Septemba 8 hadi 9 na kufungwa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Maulid Dotto kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni ‘Kukuza Umahiri katika Enzi ya Kidijitali’. “Ni siku ya kutafakari tulipotoka, tuko wapi na tunakoelekea kama jamii na taifa. Ni kuweka dhamira ya kuwaelimisha wananchi wake,” anasema Dk Ruzegea.

Dk Ruzegea anasema umahiri si katika kusoma na kuandika pekee, kwani katika karne ya 21 umahiri wa kusoma na kuandika hauishii tena kwenye karatasi na kalamu tu, bali unajumuisha pia umahiri wa kidijitali kwa maana ya uwezo wa kutumia teknolojia.

“Jamii ipende kutumia maarifa kwa ufanisi katika mazingira mbalimbali ya kijamii na kiuchumi. Kwa upande mwingine, tunahitaji jamii ya kupenda kujisomea na hii pia inasaidia kuongeza maarifa na kujenga ufahamu mpana kwa maendeleo ya mtu binafsi na kwa Taifa kwa ujumla,” anasema Dk Ruzegea.

Anasema bodi inajielekeza kukuza vipengele vyote viwili vya umahiri, yaani upande wa uwezo wa kusoma na kuandika na upande wa utamaduni na inatumia teknolojia kupata machapisho au kupata taarifa muhimu.

Dk Ruzegea anasema jukumu la TLSB ni kuendesha huduma za maktaba nchini kote bila kubagua na inatekeleza majukumu yake hayo pamoja na kuanzisha, kuziendeleza na kuhamasisha utamaduni wa kupenda kusoma hapa nchini. Anasema licha ya kutoa huduma hizo, pia wanahifadhi machapisho ya kitaifa kwa ajili ya urithi wa kitamaduni na kiakili kwa ajili ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Dk Ruzegea anasema kwa mwaka 2025/2026 bodi inaendelea na ujenzi wa maktaba mbili za mikoa ambazo zinajengwa, moja ni ya kumbukumbu ya Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli itakayoitwa John Pombe Magufuli Memorial Library na nyingine inajengwa mkoani Mwanza.

“Katika jitihada za sasa hivi za kupeleka maktaba katika jamii, tuna uhakika kabisa kwamba tutakwenda kugonga hodi katika halmashauri zetu tupewe majengo au katika vyuo mbalimbali na treni ambayo tunaweza kufanya ni maktaba za jamii,” anasema Dk Ruzegea.

Pia, ukarabati wa majengo ya zamani kwa sasa hivi unaoendelea katika mikoa ya Ruvuma, Tanga, Mara na Mtwara ili kuyaweka yawe ya kisasa na kutoa huduma kwa ufanisi. Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Maulid Dotto anasema licha ya mafanikio yaliyopatikana, hatuwezi kufumbia macho changamoto zilizopo kwani takwimu za kimataifa zinaonesha bado tuna mamilioni ya watu wazima na vijana wasiojua kusoma na kuandika.

Anasema maktaba ni kituo cha elimu endelevu na si ghala la vitabu na kuongeza kuwa, ni kituo cha ubunifu na sehemu salama kwa watoto, wanafunzi, watu wazima, vijana na watafiti. “Nimeelezwa kuwa bodi iko njiani kuanzisha maktaba za jamii. Wito wangu kwenu hakikisheni mnapeleka teknolojia za kisasa pia kwenye maktaba, ili kunufaisha umma wa Tanzania” anasema Dotto.

Naye Katibu Mtendaji wa Chama cha Wachapishaji wa Vitabu Tanzania (PATA), Abdullah Saiwaad anasema katika ulimwengu wa kidijitali, kunahitaji umahiri ili kubaki salama. Saiwaad anasema zamani taarifa na maarifa yote yamfikiayo mtu yalikuwa yamechujwa na kuthibitishwa katika vitabu.

Anasema katika ulimwengu wa kidijitali, kuna taarifa na maarifa yasiyo sahihi ambayo humwagwa mitandaoni na kufanya watu kuishia kupata taarifa zisizohitajika kwao. Saiwaad anasema utafiti uliofanywa mwaka 2025 na Unesco kuhusu hali ya uchapishaji vitabu Afrika umedhihirisha uduni wa hali ya usomaji wa vitabu Afrika kutokana na serikali nyingi kutokuhamasisha usomaji.

Naye Mwakilishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Mariam Mwinyi anasema siku ya usomaji duniani inakumbusha watu nafasi ya elimu ya usomaji katika kujenga maarifa, kukuza fikra makini na kuchochea maendeleo ya mtu binafsi pamoja na taifa kwa ujumla.

Dk Mariam anasema wizara inaendelea kuhimiza jamii nzima, hususani walimu na wanafunzi kuendeleza kudumisha utamaduni wa kusoma. Anasema kupitia jitihada zao, ni wazi kuwa Tanzania itakuwa na jamii yenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kushindana katika ulimwengu wa sasa unaobadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia na maisha ya kila siku.

Dk Mariam anasema mpango wa usomaji kidijitali ambao uko katika hatua za mwisho za kuzinduliwa utachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza utamaduni wa kusoma, kuimarisha elimu na kuendeleza maendeleo ya kijamii na kitaifa.

Anasema katika zama za kidijitali maarifa ya kimsingi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni nyenzo muhimu ya kujipatia ujuzi na kuongeza tija katika elimu. Mchapishaji wa vitabu, Yusuph Mfaume amehimiza watu kupenda kusoma vitabu ili kujua tunu za Taifa na waasisi wa Taifa la Tanzania, akiwemo Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Karume.

Mfaume anasema ili kuwajua vyema viongozi hao wakiwemo na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Rais wa Awamu ya Tano Dk John Mgufuli ni lazima kusoma machapisho mbalimbali na vitabu vyao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button