Ngajilo ahaidi ofisi yenye wasaidizi wasikivu Iringa Mjini

IRINGA: Mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo, ameahidi kuboresha ofisi ya mbunge ili iwe na watendaji wasikivu watakaopokea na kushughulikia kero za wananchi kwa ufanisi, pindi atakapochaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo hilo.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo katika kata ya Igumbilo, Ngajilo alisema ataweka mfumo utakaomuwezesha mbunge na ofisi yake kuwa karibu na wananchi kwa kipindi chote cha miaka mitano.

“Nitakuja kwenu mara nyingi sana na nitakuwa karibu nanyi. Tutakuwa na ofisi ya mbunge itakayofikika na kila mwana-Iringa. Tutateua watendaji wazuri watakaowahudumia kwa heshima na tahadhima na kushughulikia kero za makundi yote,” alisema.

Alibainisha kuwa kipaumbele chake kitakuwa kushughulikia changamoto za vijana kwa kuhakikisha wanapata mikopo ya ujasiriamali yenye riba nafuu, na kutoa elimu ya ujasiriamali ili kuwezesha vijana kujiajiri.

Vilevile, aliahidi kuwa sauti ya akina mama kwa kushughulikia kero zinazowakabili, ikiwemo tatizo la mikopo umiza, na kushughulikia changamoto za wazee katika masuala ya ustaafu na afya.

Kwa upande wa elimu, Ngajilo alisema atashirikiana na wazazi kuweka mikakati ya kuhakikisha watoto wanapata elimu bora ili kujenga kizazi chenye mustakabali imara.

Alisisitiza kuwa ili uchumi wa Igumbilo ukue, ni lazima miundombinu ifunguliwe na akataja ujenzi wa barabara ya mchepuko kutoka Tumaini hadi Igumbilo kuwa miongoni mwa miradi atakayosimamia ili kufungua zaidi uchumi wa eneo hilo.

Mgombea udiwani wa Kata ya Igumbilo, Jackson Chatanda, aliweka kipaumbele katika miradi ya ujenzi wa madarasa na kuboresha barabara za mitaa. Pia aliahidi kuanzisha mfuko wa kusaidia watoto na wazee wanaoishi katika mazingira magumu.

Aliahidi kushirikiana na uongozi kuhakikisha stendi ya mkoa inachangia mapato yatakayowezesha upatikanaji wa asilimia 10 kwa ajili ya kusaidia wazazi na familia zenye uhitaji.

Wanachama wa CCM walimshuhudia Ibrahim Gwanda akimkumbuka Ngajilo kwa mchango wake katika maendeleo ya chama, ikiwemo uwekezaji kwenye mabanda ya kitimoto na ununuzi wa magari ya UVCCM alipokuwa mwenyekiti wa vijana mkoa.

“Ngajilo ni mtu muadilifu, mnyenyekevu, hana makundi, hagawi watu. Tunahitaji mbunge ambaye watu wote kwake ni sawa,” alisema Gwanda.

Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa, Makoba, aliwataka wanachama kuhakikisha wanawashawishi wapiga kura watatu kila mmoja ili kuimarisha ushindi wa kishindo wa chama.

Ngajilo aliwaomba wananchi kumpa kura mgombea urais Dk Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea udiwani huku yeye binafsi akiahidi kuwa sauti ya wananchi wa Iringa Mjini kuanzia Septemba 29.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button