Bulala aanza kampeni kwa kishindo

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Kwimba mkoani Mwanza kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Cosmas Bulala, ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, akiwataka kuwapa kura nyingi wagombea wote wa CCM ili kuendeleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza jana kwenye uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Hungumalwa, Bulala alisema wananchi wa Kwimba wanakabiliwa na changamoto za maji, barabara, afya na miundombinu ya kijamii ambazo tayari serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeanza kuzitatua.

“Wana Kwimba mlikubaliana kwa pamoja nikawasemee changamoto zetu. Serikali ya Rais Samia tayari imeleta mradi mkubwa wa maji kutoka Mhalo kwenda Ngudu utakaonufaisha vijiji 37. Tayari fedha zimewekwa na mkandarasi ameshaanza kupokea malipo ya awali. Kufikia mwakani maji ya Ziwa Viktoria yatakuwa yamefika Ngudu,” alisema Bulala.

Bulala alisema mbali na mradi huo mkubwa, miradi mingine ya maji inaendelea kutekelezwa ikiwemo ya Buyogo, lakini akaonya kuwa baadhi ya wakandarasi wanachelewesha upatikanaji wa huduma na kuahidi kuisimamia ipasavyo endapo atachaguliwa.

Katika sekta ya barabara, alisema tayari serikali imeanza ujenzi wa madaraja na barabara ya Ngudu–Hungumalwa pamoja na ujenzi wa barabara za changarawe na madaraja mengine ikiwemo la Buyogo. Aidha, alisema katika Kata ya Hungumalwa, wananchi watapata soko jipya na stendi ya kisasa.

Akizungumzia sekta ya afya, Bulala alisema:“Mara nyingi tumekuwa tukitibiwa Misungwi kwa sababu hospitali ya Wilaya haijafanya kazi kwa ufanisi. Lakini Rais Samia ameahidi kuongeza watumishi wa afya na vifaa tiba, pamoja na kujenga vituo vya afya katika kata mbili za Kwimba.”

Kwa upande wa umeme, alisema vitongoji vyote vitapatiwa huduma hiyo ndani ya kipindi cha utekelezaji wa ilani ya CCM 2025–2030, na kuongeza kuwa wananchi wa Kwimba wamepewa kilometa sita za barabara ya lami katika makao makuu ya Ngudu.

Uzinduzi wa kampeni hizo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge, ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Viongozi wengine waliokuwepo ni mgombea ubunge wa Sumve, Moses Bujaga, madiwani wa kata zote 30 za Wilaya ya Kwimba, wagombea wa ubunge na udiwani viti maalum pamoja na viongozi wa jumuiya za CCM mkoa wa Mwanza.

Zaidi ya wananchi 7,000 walihudhuria mkutano huo mkubwa wa uzinduzi, maarufu kama ‘Kwimba Day’, na kushangilia kauli mbiu ya CCM ya kuleta maendeleo kwa vitendo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button