Ujenzi kiwanda cha meli uharakishwe -Zitto

KIGOMA: MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia Chama Cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema ujenzi wa cherezo (kiwanda) cha kutengeneza meli katika eneo la Katabe Manispaa ya Kigoma Ujiji una faida kubwa kiuchumi kwa wakazi wa Kigoma hivyo ameitaka serikali kuharakisha utekelezaji wa mradi huo ili faida ionekane kwa vitendo.
Zitto amesema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika viwanja vya Kamara Bangwe Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo amesema kutekelezwa kwa mradi huo kutainua uchumi na mzunguko wa fedha.
Amesema pamoja na faida zilizopo katika mradi huo, lakini mradi umekuwa ukisuasua kutekelezwa na kukatisha tamaa wananchi, hivyo ameitaka serikali kuyaishi maneno yake kwa vitendo.

Mwenyekiti wa Ngome ya ijana Taifa ACT Wazalendo, Abdul Nondo akizungumza katika mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge Jimbo la Kigoma Mjini Zitto Kabwe
Pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati mgombea huyo amekemea tabia ya serikali kuchukua maeneo ya watu ambayo uwekezaji unafanyika bila kulipa fidia na kwamba jambo hilo linakwenda kinyume na katiba ya nchi hivyo ametaka maeneo yanayochukuliwa lazima yalipwe fidia wakati huu ardhi inapanda thamani na watu wanaona ardhi hizo kama mitaji yao.
Zitto amesema kuwa Ili kukabiliana na ucheleweshaji huo anahitajika mbunge ambaye atasimama ni kuipigia kelele serikali kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa wakati hivyo amewaomba wananchi wa jimbo hilo katika uchaguzi wa Oktoba 29 mwaka huu.

Mgombea ubunge Jimbo la Kigoma Mjini Zitto Kabwe (kulia) ACT Wazalendo akimnadi mgombea udiwani wa kaya Bangwe, Abdallah Rajab Mandanda
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ngome ya vijana Taifa ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesema kuwa Mkoa Kigoma unahitaji wabunge wanaoweza kupambana na kujenga hoja na kusimamia kwa karibu kuhakikisha miradi inatekelezwa.
Nondo amesema kuwa kwa sasa miradi mikubwa inatekelezwa Kigoma ukiwemo mradi wa reli ya kisasa (SGR) hivyo ni lazima mkoa upate wabunge watakaoweza kusimamia fedha hizo zifanye kazi bila kuchepushwa au kuwepo kwa matumizi mabaya hivyo akataka Zitto Kabwe achaguliwe akasimamie hilo.



